• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
COTU yapinga uteuzi wa Karangi kusimamia NSSF

COTU yapinga uteuzi wa Karangi kusimamia NSSF

Na Wanderi Kamau

MUUNGANO wa Kitaifa wa Wafanyakazi (COTU) umepinga uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Mstaafu Julius Karangi kama mwenyekiti wa bodi ya Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Bw Karangi aliteuliwa wiki iliyopita na Waziri wa Leba Ukur Yattani kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, kuchukua nafasi ya Gideon Ndambuki baada ya kipindi chake kumalizika mnamo Februari.

Uteuzi wake tayari ushachapishwa katika gazeti rasmi la serikali, toleo la wiki iliyopita, huku ukitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.

Lakini Jumanne, COTU ilikosoa uteuzi huo, ikiutaja kuwa njama za serikali kuwaondoa Katibu wake Mkuu Francis Atwoli na Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waajiri Kenya (FKE) kama wanachama wa bodi ya hazina hiyo.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza wa muungano huo, Earnest Nadome alisema kwamba wana habari kwamba kuna njama za kuwaondoa wawili hao “ili kuwanyang’anya udhibiti wa bodi hiyo.”

“Tuna habari kwamba lengo kuu la uteuzi wa Bw Karangi kama mwenyekiti wa hazina hii ni kuanza mchakato wa kutupokonya udhibiti wa uongozi wa hazina hii, licha ya Bw Atwoli na Bi Mugo kuwakilisha matakwa ya wafanyakazi kote nchini,” akasema Bw Nadome.

Mbali na hayo, Bw Nadome alisema kuwa watatumia njia zote kuhakikisha wawili hao wanabaki, kwani kuondolewa kwao ni sawa na “kuwanyamazisha wafanyakazi.”

“Hatuwezi kuketi kitako wakati serikali inapanga njama za kutunyamazisha kimakusudi,” akasema.

Uteuzi wa Bw Karangi unajiri huku hazina ikiandamwa na msururu wa sakata za rushwa zinazojumuisha kupotea kwa mabilioni ya fedha.

Mojawapo ya sakata hizo ni ununuzi tata wa hisa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) mnamo 2016, ambapo inahofiwa kwamba ilipoteza hadi Sh1.6 bilioni katika hali tatanishi.

Aidha, NSSF inadaiwa kutumia kampuni ya Discount Securities Limited (DSL) kununa hisa hizo, ila taratibu zilizofuatwa hazikuwa wazi.

Hilo lilipelekea baadhi ya maafisa wake wakuu kufunguliwa mashtaka, ila wamepinga madai hayo.

Hazina hiyo pia inakumbwa na mradi tata wa ujenzi wa Tassia, ambapo inadaiwa kwamba ilipoteza hadi Sh5 bilioni.

Hata hivyo, hazina imejitetea, ikidai kwamba kila taratibu zilifuatwa katika uendeshaji wa mradi huo.

You can share this post!

Pabaya kwa kutumia barua feki ya ulemavu kuomba viza ya...

Yaya wa Wanjigi ana kesi ya kujibu – Mahakama

adminleo