• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Walimu wafumaniwa lojing’i wakiwa na wanafunzi

Walimu wafumaniwa lojing’i wakiwa na wanafunzi

Na JADSON GICHANA

Maafisa wa Polisi eneo la Nyamache, Kaunti ya Kisii wameanzisha uchunguzi kubaini kisa ambapo walimu wawili walidaiwa kupatikana wakiwa na wanafunzi wao kwa lojing’i.

Walimu hao walipatikana kwenye lojing’i tofauti wakiwa na wanafunzi kwenye jumba moja la starehe katika eneo hilo.

Inadaiwa kuwa wawili hao walitoroka baada ya makahaba waliokuwa humo kulalamika kuwa wameachwa na wanaume hao na kuchukua wanafunzi wa shule.

“Hawa wawili waliingia kwa gesti saa kumi na mbili jioni na nikashangaa sana kuwaona kwa vile sisi tuko hapa na hakuna mwanamume yeyote anatuona,” alisema kahaba ambaye hakutaka jina lake kutajwa.

Wawili hao ni walimu katika shule moja ya msingi ambapo walitenda kitendo hicho baada ya kushiriki michezo ya katika shule jirani, Kaunti ndogo ya Nyamache. Wakiwa njiani kurudi shuleni mwao waliwapeleka wanafunzi hao wawili wa darasa la nane kwa baa.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo alisema kuwa wanafunzi hao walikuwa miongoni mwa wengine walioshiriki michezo hiyo na walimu ndio walikuwa wakiwasimamia.

“Niliwaruhusu wanafunzi na walimu kuelekea katika mashindano ya michezo jana asubuhi, lakini kufikia jioni mwendo wa saa moja nikapigiwa simu kuwa wanafunzi wangu wamepatikana kwa lojing’i wakiwa na walimu wao,”alisema mwalimu mkuu huyo tunayembana jina kwa sababu za kisheria.

Alisema kuwa wanafunzi hao walipelekwa kwa baa wakiwa na sare za shule hiyo.

Mkurugenzi wa idara ya Elimu katika Kaunti hiyo Dkt William Sugut alisema kwamba alipokea habari hizo kwa mshangao mkubwa kwa vile walimu hao walipewa wanafunzi kuwapeleka katika michezo na kuwarudisha makwao.

Alisema kuwa tayari walimu hao wamesimamishwa kazi ili uchunguzi ufanywe kwa kina.

“Maafisa wa polisi na wa Elimu wameanzisha uchunguzi kubaini kisa hicho na idara ya kuajiri walimu imewasimamisha kazi wawili hao,” alisema Dkt Sugut.

Dkt Sugut aliwaonya walimu ambao wanaharibu wanafunzi kwa kushiriki ngono na wanafunzi kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha, mkurugenzi huyo alieleza kuwa hata ingawa walitoroka mkono wa sheria utawapata na watashtakiwa punde tu watakaponaswa.

“Hata ingawa walitoroka, mwishowe watapatikana na idara itawachukulia hatua,” akasema.

Akithibitisha kisa hicho OCPD wa eneo la Nyamache Japheth Mwirichia alisema kuwa waalimu wawili na wanafunzi wawil wasichana walipatikana kwa lojingi kwenye baa moja katika eneo. Baada ya makahaba walianza kuwapigia kelele walitoroka.

Alisema kuwa polisi wameanzisha msako mkali ili kuwatafuta wawili hao ambao walitoroka na kujificha .lakini wakinaswa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Tulipata ripoti kutoka kwa mwenye baa hiyo kuwa wanaume wawili ambao walidaiwa kuwa waalimu na wanafunzi wawili walikuwa wamevaa sare za shule wamepatikana kwa lojingi ya baa moja ,waliposikia kuwa polisi wamo njia kukuja wakatoroka,”alisema Bw Mwirichia.

“Maafisa wa polisi wameanzisha msako mkali ili kuwatafuta waalimu hao na wakikamatwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,”alisema.

You can share this post!

Maafisa wa kaunti waingia mafichoni kuhepa kukamatwa na EACC

Mwanamke alilia polisi waachilie mume aliyenajisi binti yake

adminleo