• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:55 AM
Joho amkaribisha Uhuru Mombasa kwa shangwe

Joho amkaribisha Uhuru Mombasa kwa shangwe

Na KAZUNGU SAMUEL

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho Alhamisi alimkaribisha Mombasa Rais Uhuru Kenyatta kwa mbwembwe na kuhitimisha uhasama wao wa kisiasa uliotawala miaka ya nyuma.

Gavana huyo aliyekuwa amevalia kanzu nyeupe alipigana pambaja na Rais Uhuru Kenyatta mbele ya viongozi wengi wa serikali kuu na wabunge wa Pwani katika kile ambacho kiliashiria mabadiliko ya siasa tangu muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta and kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga mwezi wa Machi mwaka huu.

Viongozi hao wawili walifungua rasmi utumaiji wa barabara ya kisasa ya Dongo Kundu katika eneo la Miritini.

Katika hafla hiyo, Gavana Joho aliahidi kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta kwa ajili ya maendeleo katika kaunti na taifa lote kwa jumla.

“Mimi niko tayari na tutafanya kazi na wewe kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” akasema Gavana Joho.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Gavana Joho na Rais Uhuru Kenyatta kuonekana pamoja kwenye miradi tangu Gavana Joho kuzuiliwa kuambatana na Rais alipozuru Pwani mwaka jana kuzindua miradi ya maendeleo.

“Nyote mnaniona hapa. Mara nyingi mimi sikuwa nikihudhuria hafla kama hizi kwa sababu ya vuta nikuvute iliyokuwepo.

“Tulikuwa tukisikiliza viongozi mbalimbali. Lakini leo hii mimi niko hapa na nitaendelea kuhimiza amani baada ya baba (Raila Odinga) kufanya hivyo,” akasema huku akishangiliwa.

Gavana Joho alikuwa ameandamana na wabunge wa Pwani na alionekana mchangamfu sana huku akitaniana na viongozi kadhaa kabla ya kuwasili kwa Rais Kenyatta kufungua barabara hiyo.

Miongoni mwa viongozi waliokuwepo walikuwa ni pamoja na gavana wa Kwale Salim Mvurya, katibu wa ardhi Gideon Mung’aro, na aliyekuwa mshirikishi wa kanda ya Pwani Bw Nelson Marwa.

Wabunge Abdulswamad Nassir (Mvita), Badi Twalib (Jomvu), Omar Mwinyi (Changamwe) pamoja na wabunge wengine wa Pwani akiwemo Khatib Mwashetani (Lunga Lunga) walikuwemo.

Hatua ya Gavana Joho kumlaki Rais Kenyatta ilikuwa imefuatiwa na mwafaka huo wa amani kati ya Raila na Uhuru ambapo Joho alisema kuwa anauunga mkono na kuushabikia.

Wakati wa sherehe za sikukuu ya Madaraka, Gavana Joho aliwaambia wakazi wa kaunti ya Mombasa katika uwanja wa Tononoka kwamba aliamua kuhudhuria sherehe hizo kwa sababu ya mwafaka huo.

Mwaka jana Gavana Joho alikatazwa kuhudhuria hafla za kuzinduliwa kwa fewri mpya ya Mtongwe ambayo Rais alikuwa akizindua kutokana na tofauti kali za kisiasa.

Siku hiyo Gavana Joho alizuiliwa na maafisa wa kikosi maalum cha kumlinda Rais katika daraja la Nyali katika kisa ambacho kilivutia watumiaji wengi wa barabara hiyo. Baadaye Gavana Joho alidai kwamba alizuiliwa kuhudhuria hafla hiyo kwa dai alikuwa mpinzani wa Rais Uhuru Kenyatta.

Lakini hapo jana, alikuwa alionekana kutangamana na kila kiongozi aliyekuwa katika eneo ambalo Rais alizindua barabara hiyo mpya nay a kisasa kabla ya kumpokea rasmi Rais Uhuru Kenyatta katika jiji la Mombasa.

Picha za Rais Uhuru Kenyatta akipigana pambaja na Gavana Joho zilianza kutumwa mitandaoni punde tu baada ya kuchukuliwa na kuanza kuvutia hisia mbalimbali za wakazi wa Pwani kwenye mitandao.

You can share this post!

BAJETI YA KUNYONYA: Raia kuumia zaidi

Ruto anyooshea Kalonzo mkono wa ushirikiano

adminleo