Michezo

Ni kicheko tu kwa Morocco kuona Saudia ikinyeshewa 5-0 na Urusi

June 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

SAA chache baada ya Saudi Arabia kukosa kipigia kura ya kuamua mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2026, Morocco imechekelea nchi hiyo kupapurwa 5-0 na wenyeji Urusi katika makala ya mwaka 2018.

Saudi Arabia iliipa Amerika Kaskazini (Marekani, Canada na Mexico) kura yake na kuisaidia kushinda Morocco kwa kura 134-65 Juni 13, 2018.

Baada ya uchaguzi huo kufanywa jijini Moscow, Morocco ililaumu Saudi Arabia kwa masaibu yake ikiitaja kama msaliti na kusema iliongoza mataifa ya Bara Asia hasa ya Kiislamu kupigia Amerika Kaskazini kura badala ya kuiunga mkono.

Hata hivyo, Morocco inaonekana ilipata kisasi chake wakati timu ya Saudi Arabia ilipofunzwa jinsi ya kusakata soka katika mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Urusi.

Baada ya Saudi Arabia kupokea kichapo hicho kikali kupitia mabao ya Yury Gazinsky, Artem Dzyuba, Aleksandr Golovin na mawili kutoka kwa Denis Cheryshev, Wamoroko hawakuficha furaha yao.

“Tulitamani sana muwe na mwanzo mzuri kama huo,” gazeti moja nchini Morocco lilinukuu mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wakifurahia uchungu wa Saudi Arabia kuaibishwa. Saudi Arabia itakutana na Uruguay katika mechi yake ya pili Juni 20 kabla ya kukamiliosha mechi za Kundi A dhidi ya majirani Misri mnamo Juni 25.

Atlas Lions ya Morocco iko katika Kundi B. Itaanza kampeni yake dhidi ya Iran hapo Juni 15, ivaane na Ureno mnamo Juni 20 na kufunga raundi ya kwanza na mechi dhidi ya Uhispania mnamo Juni 25.