• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
JUBILEE YAPONDA RAILA: ‘Baba’ naye amjibu Ruto akome ‘kubwekabweka’ na ‘kutangatanga’

JUBILEE YAPONDA RAILA: ‘Baba’ naye amjibu Ruto akome ‘kubwekabweka’ na ‘kutangatanga’

VALENTINE OBARA, MOHAMED AHMED na DPPS

VIONGOZI wa Chama cha Jubilee Jumapili walimshambulia Kiongozi wa ODM Raila Odinga, hatua ambayo inazua masuala kuhusu kujitolea kwa wanasiasa katika kufanikisha maridhiano baina ya Wakenya.

Vigogo hao wa Jubilee waliojumuisha magavana, seneta na wabunge walimwamia Bw Odinga akome kumkashifu Naibu Rais William Ruto kuhusu siasa za 2022.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga naye alimrushia makombora Bw Ruto akimwambia aache “kutangatanga” na “kubwekabweka”akifanya kampeni za 2022 .

Bw Odinga na naibu wake Hassan Joho walitaja ziara nyingi za Bw Ruto kama kampeni za mapema.

“Wacha kurandaranda hapa na pale, kutangatanga ati wewe unasema mimi nitakuwa Rais mwaka 2022. Unajuaje hilo? Ni Wakenya ambao wataamua yule ambaye watamchagua rais wao,” akasema Bw Odinga.

Nao viongozi wa Jubilee wakiongea mjini Thika walidai Bw Odinga ana njama ya kuvuruga chama chao cha Jubilee na kumtaja kama ‘asiye na adabu’.

Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, alikosoa jinsi Bw Odinga alivyopuuzilia mbali ziara za Bw Ruto katika ngome zake za kisiasa na kuzifananisha na kampeni za mapema.

Kulingana na Bw Kindiki, chama cha Jubilee hakina haja ya kufanya kampeni kwa sababu wanachama wanaamini Bw Ruto ndiye atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapokamilisha hatamu yake ya pili ya uongozi mwaka wa 2022.

“Jubilee haifanyi kampeni za 2022 wala mwaka mwingine wowote, bali tunazuru mashinani kutafuta jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba wananchi. Bw Ruto ndiye mgombeaji wetu bila pingamizi atakayechukua mamlaka wakati Rais Kenyatta atakapostaafu mwaka wa 2022 pamoja na Bw Odinga,” akasema Prof Kindiki.

Magavana waliokuwepo ni Ferdinand Waititu na naibu wake James Nyoro, Granton Samboja (Taita Taveta) na Muthomi Njuki (Tharaka Nithi).

Baadhi ya wabunge waliomtetea Naibu Rais ni Kimani Ichungwa (Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Jude Njomo (Kiambu Mjini) Githua Wamashukuru (Kabete), Patrick Wainaina (Thika Mjini), miongoni mwa wengine.

Bw Waititu alidai kuwa Bw Odinga si mwaminifu katika juhudi za kuleta umoja wa taifa kwani anadunisha hatua za viongozi wengine kueneza umoja huo mashinani.

Kwa upande wake, Bw Ichungwa alishangaa kwa nini Bw Odinga anakashifu ziara za Bw Ruto ilhali yeye ndiye aliambia Wakenya waungane baada ya kusalimiana na Rais Kenyatta.

“Si jukumu lake kutuambia kile tunafaa kufanya kuhusu uongozi wa nchi hii. Tuna imani kwa uongozi wa Rais Kenyatta na Naibu Rais,” akasema.

Bw Ruto amekuwa akizuru pembe tofauti za nchi katika siku za hivi majuzi kwa kile anachodai ni juhudi za kukagua miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali mashinani na kupeleka maendeleo zaidi kwa wananchi.

 

Ni mapema mno 

Hata hivyo, ziara hizo zimetazamwa kama juhudi za kujiandaa kwa uchaguzi wa urais wa 2022, huku Bw Odinga akisisitiza bado ni mapema mno kuanza kufikiria kuhusu uchaguzi ujao.

Naibu Rais jana aliepuka mijadala hiyo na kusema serikali imejitolea kufanikisha umoja na maendeleo ya nchi ambayo yatapewa kipaumbele kuliko masuala mengine yote.

Aidha, Bw Odinga aliendelea kumchapa kwa maneno Bw Ruto kuhusiana na ziara zake ambazo ameonekana akihudhuria na kutoa michango ya fedha.

“Kisha watu wanaenda wakipeana pesa hapa, mara kule na tunajua mshahara wanaopata. Ndio maana tunasema wale ambao wanaiba mali ya umma wanajulikana kutokana na vile wanatembea na sura zao zinaonyesha,” akaongeza Bw Odinga huku akisifia tangazo la rais kuhusiana na ukaguzi wa mali ya watumishi wa umma.

Bw Odinga alisifu Rais Kenyatta kwa tangazo lake kuhusu utathmimi wa mali ya maafisa wa Serikali.

“Katika vita dhidi ya ufisadi tutasimama na serikali kuona vinapiganwa mpaka mwisho, na wale wanaohusika katika wizi wa mali ya umma wakamatwe na kutupwa korokoroni,” akasema Bw Odinga.

 

Ukaguzi wa wafanyakazi serikalini 

Katika ziara yake wiki iliyopita wakati wa ufunguzi rasmi wa barabara ya kisasa ya Dongo Kundu, Rais Kenyatta aliapa kupigana na ufisadi na kutangaza kuwepo kwa ukaguzi wa wafanyakazi wa umma ukiongozwa na yeye.

Bw Kenyatta alisema atakuwa wa kwanza kufanyiwa ukaguzi huo wa mali anazomiliki akifuatwa na naibu wake, halafu magavana na mawaziri pamoja na wafanyakazi wengine.

Hapo jana wakati wa sherehe za Idd Baraza ambapo Bw Joho alikuwa ameandamana na Bw Odinga katika eneo la Treasury Square jijini Mombasa, aliunga mkono mwito wa Bw Kenyatta na kusema watasimama pamoja kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Vile vile, kiongozi huyo alipendekeza kuwa ukaguzi wa mali wanazomiliki viongozi ufanywe na mashirika ya kimataifa ambayo hayataweza kushawishika.

“Nilisema hapa mwaka jana kuwa viongozi tufanyiwe ukaguzi huu na mimi naomba sisi viongozi kuanzia rais na naibu wake na magavana tufanyiwe zoezi hilo na wakaguzi wa kimataifa na wale wengine wafanyiwe hapa hapa,” akasema Bw Joho.

Bw Joho pia hakusita kueleza azma yake ya kuwania kiti cha urais 2022.

“Sisi tunataka kuwambia wale ambao wameanza kampeni mapema kuwa hawana mkataba na Mwenyeezi Mungu. Tunasubiri muda mwafaka ufike na watakiona cha mtema kuni,” akasema.

You can share this post!

Jeshi la Uganda lazidi kuhangaisha Wakenya Ziwa Victoria

Al Shabaab waua polisi 8 kwa bomu Wajir

adminleo