KURUNZI YA PWANI: Uchu wa mali, tuhuma za uchawi zinavyowaangamiza wazee Kilifi

Na KAZUNGU SAMUEL

Baada ya mvi kuwa chanzo cha mauaji ya wazee katika kaunti ya Kilifi miaka ya awali, mambo sasa ni tofauti.

Taifa Leo imegundua kwamba chuki ya watoto kutaka kurithi mali za baba zao sasa ndio jambo ambalo linapeleka vijana kutaka kuwaangamiza.

Baadhi ya wazee tulioongea nao hivi majuzi katika kaya Godhoma walitoa picha ya kutisha kuhusu kuibuka kwa mbinu mpya za kuwaangamiza.

Mmoja wa wahasiriwa hawa ni Mzee Samwel Nyiro mwenye umri wa miaka 67. Yeye aliponea kifo mwaka wa 2014 baada ya kuvamiwa na kukatwakatwa kijijini kwake eneo la Ngerenya, kaunti ya Kilifi.

Wauaji hao kulingana na mzee huyo walitaka kumwangamiza kwa dai alikuwa anairoga familia yake na alikuwa mkosi katika kijiji hicho.

“Ni Mungu tu ndiye aliyeniokoa lakini kwa sasa ningekuwa marehemu,” akasema katika kijiji cha Kaya Godhoma ambako alijificha kuepuka mautu baada ya kutoka hospitalini.

Hata hivyo baada ya kuachiliwa hospitalini, mzee huyo alilazimika kutorokea kwa kakake ili kuuguza vidonda baada ya kupatiwa taarifa kwamba alikuwa anasubiri kuuawa nyumbani kwake pindi tu atakaporudi.

Mhasiriwa huyu alisema kuwa suala la kuwa mrogi lilipandwa na chuki za kifamilia baada ya kukataa kuruhusu uuzaji wa shamba la ekari 12 ambalo analisimamia kama mtoto mkubwa katika boma.

“Mimi ndiye mkubwa katika familia yetu na nilipewa jukumu na marehemu wazazi wetu nilinde shamba hilo kwa ajili ya kizazi kijacho. Lakini kuna binamu yangu ambaye alitaka kuuza lakini nikakataa.

Hapo ndipo mpango uliwekwa wa kuniangamiza ili uuzaji wa shamba uendelee,” akasema katika mahojiano. Aidha alisema kwamba kwa sasa anahofia kurudi kijijini kusimamia shamba hilo ingawa bado halijauzwa.

“Lengo lao ni kuhakikisha kwamba nimeuawa ili wapate nafasi ya kuuza shamba. Hio ndio sababu kuu ambayo ilinifanya nitorokee hapa Kaya godhoma. Ni shamba tu ndilo ambalo naamini linataka kunipeleka kaburini,” akasema Mzee Nyiro.

Katika tukio lengine la kusikitisha na kuogofya, mzee Duni Nzai mwenye umri wa miaka 85 alilazimika kuacha jeneza la marehemu mkewe na kutoroka watu walipotaka kumuua. Walidai kwamba alikuwa amemroga mkewe na alikuwa na mkono katika kifo chake.

“Jambo ambalo wale waliotaka kuniua hawakujua ni kuwa niliuza sehemu ya shamba langu ili kumuuguza mke wangu,” akasema huku akitokwa na machozi.

Alisema kuwa hata baada ya kuokolewa mikononi mwa mwa wauaji, hafikirii kurudi kijijini kwake kwa sababu kuna binamu zake ambao alidai wanataka kuuza shamba. “Mimi sioni salama nikiwa nje ya kituo hiki. Kisa na maana ni shamba ambalo binamu zangu wanataka kuliuza. Mimi nimekataa kabisa na ndio maana nilisingiziwa kwamba ni mchawi.

Siwezi kuroga mtu ila ninajua kwamba huu ni mpango kabambe wa kuniangamiza. Sitarudi huko,” akasema.

Kwa Mzee Kahindi Ngoka mwenye umri wa 84, maisha kwake pia ni ya taabu na mahangaiko.

Alitorokea kituo hiki cha Kaya Godhoma miaka saba iliyopita kutoka kwao Tsangalaweni.Kisa na maana ni kuwa mkewe na watoto walipanga njama za kumuua wakisema kuwa ni mchawi.

“Baada ya kuponea kifo, niliunganishwa na marehemu Mangi Mitsanze ambaye alikuwa akisimamia kituo hiki kabla afariki,” akasema mzee huyo.

Hata hivyo alisema jambo ambalo limemtatiza zaidi ni mpango wa familia kutaka kuuza shamba lake la ekari 10.

 

Kusingiziwa uchawi

“Mke wangu anataka kuuza shamba akishirikiana na watoto wangu. Kwa sababu mimi mwenyewe sitaki, wananisingizia kwamba mimi ni mchawi. Sasa kama mimi ni mchawi, waachane na shamba yangu basi,” akasema kabla ya kuanza kulia wakati wa mahojiano.

Mauaji haya ya wazee yameendelea kuwa kero katika kaunti hiyo lakini jambo ambalo limeanza kujitokeza ni uchu wa watoto kuamua kuuza mashamba kwa taamaa ya kupata pesa.

Mbunge wa Ganze ambako kituo hicho kinapatikana Bw Teddy Mwambire alisikitishwa na aina hii mpya ya kuwaua wazee na kuahidi kushirikiana na maafisa wa usalama kuhakikisha jambo hili limepata suluhisho la kudumu.

“Kwa muda mrefu, eneo la Ganze linajulikana sana kwa mauaji ya wazee hawa na tumeanza kugundua kwamba sio masuala ya mvi tena ila ni kuhusu unyakuzi wa mashamba na migogoro ya familia.

Sasa kilichoko hapa ni kuhakikisha kwamba jambo hili linapata suluhu ya kudumu,” akasema mbunge huyo.

Ripoti ya usalama inaonyesha kuwa mwaka wa 2014 pekee jumla ya wazee 108 waliuawa katika kaunti ya Kilifi na mwaka wa 2015, jumla ya wazee 104 waliuawa.

Kamishna wa kaunti ya Kilifi Bw Magu Mutindika tayari ameonya kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa familia endapo mmoja wao atapatikana ameauwa.

Habari zinazohusiana na hii

Pwani kuenda kortini