HabariSiasa

Waiguru atisha kumshtaki Jicho Pevu kwa kumhusisha na wizi NYS

June 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru ametisha kumshtaki Mbunge wa Nyali Mohammed Ali kwa kumhusisha na sakata ya wizi wa Sh9 bilioni NYS.

Bi Waiguru ametoa makataa ya siku saba kwa mbunge huyo awasilishe msamaha kwa maandishi la sivyo amfungilie mashtaka.

Bw Ali, maarufu kama Jicho Pevu, pia alipendekeza kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Ndegwa Muhoro pia achunguzwe kuhusiana na sakata hiyo.

Mbunge huyo aliorodhesha kampuni 40 ambazo alisema zinapasa kuchunguzwa kwa kuhusika moja kwa moja na sakata hiyo

“Tumepewa agizo kwamba ikiwa hautaondoa matamshi hayo na kuomba msamaha ndani ya muda wa siku saba tutaanzisha mashtaka dhidi yako ambayo yatakugharimu pakubwa,” wakili wa Bi Waiguru Mohammed Muigai alisema Alhamisi kwenye taarifa Jumanne.

Kulingana na Waiguru maneno yaliyotumiwa na Bw Ali yaliashiria kuwa yeye ni m mwizi na mnyakuzi wa pesa za umma, kando na kutostahiki kushikilia afisi ya umma.

“Mteja wetu amesema maneno ambayo yalitumiwa yalilengwa kumharibia sifa na kumwondolea heshima ilhali yeye ni afisa wa umma anayeheshimika,” taarifa hiyo ikaongeza.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Jumanne Bw Ali pia aliwaambia mawaziri Mwangi Kiunjuri, Sicily Kariuki na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa Samsom Muchuki wajitokeze waelezee kile wanachojua kuhusu sakata hiyo.

“Kiunjuri na Kariuki wamewahi kuhudumu katika Wizara hii ambayo inasimamia NYS. Kwa hivyo, wanafaa kujitokeza na kuelezea kile wanachojua kuhusu sakata hii,” akasema Bw Ali ambaye alikuwa ameandamana na wenzake, Tindi Mwale (Butere) na Caleb Amisi.

Wabunge hao waliwataja washukiwa waliokamatwa kuhusiana na sakata hiyo kama samaki wadogo.

“Tungetaka papa na nyangumi pia wakamatwe ili tuwe na matumaini kwamba serikali inajituma katika vita hivi dhidi ya ufisadi,” akasema Bw Amisi ambaye ni Mbunge wa ODM.

Wabunge hao walisema hayo saa chache baada ya Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Utumma, Vijana na Jinsia Lilian Mbogo Omollo, Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai na washukiwa wengine 41 kuachiliwa huru kwa dhamana ya Sh1 milioni kila mmoja.

Hii ni baada ya wao kukaaa korokoroni kwa zaidi ya wiki tatu.