• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Wabunge wamkemea Waiguru kuwatisha kwa kumhusisha na ufisadi NYS

Wabunge wamkemea Waiguru kuwatisha kwa kumhusisha na ufisadi NYS

Na CHARLES WASONGA

Mbunge wa Shinyalu Justus Kizito amemkaripia Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kwa kutisha kuwashtaki wabunge ambao walimhusisha na sakata ya wizi wa mabilioni ya pesa za umma katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).

Akiongea na wanahabari Jumatano katika majengo ya bunge Bw Kizito alisema wabunge ambao walilengwa na Bi Waiguru hawatamwomba msamaha jinsi alivyotaka kwani walikuwa wakifanyakazi kazi yao ya kulinda mali ya umma na? kupambana na ufisadi.

“Waiguru anafaa kuelewa kuwa Katiba ya Kenya inawapa wabunge mamlaka ya kuchunguza masuala yenye umuhimu kwa taifa. Na wizi wa Sh9 bilioni na Sh791 milioni katika NYS sio masuala mepesi.

Kwa hivyo, Waiguru hafai kuwatisha wabunge wanapofanya kazi yao ya kutaka yeye na watu wengine waliosimimia shirika hilo wachunguzwe,” akasema Mbunge huyo wa ODM huku akimhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kuwa wanaounga mkono vita dhidi ya ufisadi.

“Waiguru anafaa kutisha Wakenya wanaolalamikia wizi wa pesa zao chini ya usimamizi wake wala sio sisi. Wakenya wamepoteza jumla ya Sh10 bilioni kupitia NYS na wahusika wote wanafaa kuadhibiwa bila huruma,” akaongeza Bw Kizito.

Aliandamana na wabunge; Justus Kizito (Shinyalu, ODM), Alpha Miruka (Bomachoge Chache, KNC), Tindi Mwale (Butere, ANC) na mbunge maalum Sammy Saroney (Wiper).

Mnamo Jumanne Bi Waiguru alitoa makataa ya siku saba kwa Bw Ali, na wenzake, kumwomba msamaha, kwa maandishi, la sivyo, awafungulie mashtaka mahakamani kwa kumharibia jina.

“Tumepewa agizo kwamba ikiwa hautaondoa matamshi hayo na kuomba msamaha ndani ya muda wa siku saba tutaanzisha mashtaka dhidi yako, na wenzako,” wakili wa Bi Waiguru Mohammed Muigai alisema Jumanne kwenya taarifa.

Kulingana na Waiguru maneno yaliyotumiwa na Bw Ali dhidi yake yaliashiria kuwa yeye ni mwizi na mnyakuzi wa pesa za umma, kando na kutostahiki kushikilia afisi ya umma.

Wabunge wengine aliowalenga ni; Mbw Mwale, Caleb Amisi (Saboti, ODM) na Kuria Kimani (Molo, Jubilee).

 

Wanaofaa kuchunguzwa kwa wizi NYS

Wabunge hao walikuwa wamedai kuwa Bi Waiguru, aliyekuwa Mkuugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Ndegwa Muhoro, Waziri wa Afya Sicily Kariuki na mwenzake Mwangi Kiunjuri (Kilimo) wanapasa kuchunguzwa kuhusiana na wizi wa Sh9 bilioni katika NYS.

Bi Waiguru alikuwa waziri wa Ugatuzi na Mipango sakata ya kwanza ya kupotea kwa Sh791 milioni katika NYS. Bw Kinjuri na Bi Kariuki pia waliwahi kushikilia wadhifa huo baada Waiguru kujiuzulu kutokana na shinikizo za umma.

Wabunge hao pia walipendekeza kuchunguzwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NYS Nelson Githinji na naibu wake Sam Michuki, Inspekta wa Polisi Julius Muia, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Petro Kenya Oil Gor Semelang’o pamoja na wafanyabishara Ben Gethi na Peter Gathecha.

Akiongea kuhusu vitisho vya Bi Waiguru Bw Ali, maarufu kama “Jicho Pevu” alisema: “Tunamwogopa Mungu pekee. Hatumwogopi Waiguru. Vitisho vyake ni bure… aende mahakamani alivyotisha. Hatuwezi kusuluhisha awamu ya pili ya sakata ya NYS bila kuangazia sakata ya kwanza. Ikiwa Waiguru ni msafi mbona anaingiwa na wasiwasi?”

“Nimetumwa bungeni na watu wa Nyali kutetea wizi wa pesa wanazolipa kama ushuru kwa serikali. Kwa hivyo, sitaogopa vitisho kutoka kwa mtu yeyote na sitaomba msamaha kwa kutaja majina ya watu wakubwa kama Waiguru na wengineo katika sakata hii ya NYS,” akaongeza mbunge huyo ambaye hakuchaguliwa kwa tiketi ya chama chochote bungeni.

You can share this post!

Msiingize siasa kwa sukari ya sumu, wanasiasa waonywa

Wabunge wakerwa kupimiwa samaki mkahawani

adminleo