• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Watalii 7,000 watarajiwa kunogesha biashara Lamu

Watalii 7,000 watarajiwa kunogesha biashara Lamu

NA KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya watalii 7000 wanatarajiwa kuzuru eneo la Lamu katika kipindi cha ziara nyingi za watalii kinachotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.

Waziri wa Utalii, Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu, anasema hatua hiyo inatokana na imani ambayo imerejeshwa kwa watalii hasa baada ya usalama kudhibitiwa kote Lamu.

Sekta ya Utalii ya Lamu imekuwa ikipokea changamoto tele hasa tangu Al-Shabaab walipovamia na kuua wakazi zaidi ya 100 kwenye miji ya Mpoeketoni, Kibaoni, Witu na Hindi kati ya 2014 na 2015.

Akizungumza wakati wa kongamano la washikadau kwenye hoteli ya Majlis eneo la Shella Alhamisi, Bw Mwasambu aliwashauri wenye mahoteli kote Lamu kujiandaa vilivyo ili kupokea watalii wengi zaidi kutoka kutoka sehemu mbalimbali za nchi na ng’ambo punde Julai itakapoanza.

Mmiliki wa hoteli ya Bush Gardens, Ghalib Alwy akiwa na wafanyakazi wake hotelini wakiendeleza ukarabati wa hoteli hiyo. Asema anatumaini kunoga kwa biashara hiyo ifikapo Julai. Picha/ Kalume Kazungu

“Ningewashauri wenye hoteli kutengeneza mahoteli yao vizuri na hata kupanua hoteli hizo mapema ili kukimu idadi kubwa ya wageni tunaotarajia kupokea eneo hili kuanzia Julai. Tunatarajia zaidi ya watalii 7000 wa hapa nchini na ng’ambo kuzuru eneo hili msimu wa Julai hadi Disemba,” akasema Bw Mwasambu.

Baadhi ya wadau wa utalii waliohojiwa na Taifa Leo kwenye miji mbalimbali ya Lamu walieleza matumaini ya kunoga kwa biashara hiyo punde Julai itakapofika.

Wamiliki wa mahoteli kwenye miji ya Lamu, Ras Kitau, Shella, Manda, Mkokoni, Kiwayu, Matondoni, Kipungani na viungani mwake tayari wameanza kukarabati hoteli zao ilhali wengine wakizijenga upya ili kuvutia watalii wanaotarajiwa kuwa wengi msimu wa Julai.

Bw Ghalib ALwy ambaye anamiliki hoteli ya Bush Gardens mjini Lamu anasema wameanza kupokea kodi ya vyumba vya kulala kwa watalii kutoka ng’ambo mapema ikilinganishwa na miaka ya kawaida.

Alisema hiyo ni dalili tosha kwamba biashara ya utalii itanoga mwaka huu.

Asema wamezindua kampeni ya kusafisha fuo za bahari na hata kuelimisha umma wa Lamu kuepuka kutupa ovyo taka kwenye fuo. Picha/ Kalume Kazungu

“Tunasubiri kipindi cha Julai kufika. Tayari tumepokea kodi za mapema kwenye hoteli zetu kwa watalii wa ng’ambo ambao wanazuru Lamu ifikapo mwezi Julai. Tunaishukuru serikali ya kitaifa kwa juhudi zake kudhibiti usalama eneo hili la Lamu,” akasema Bw Alwy.

Naye mmiliki wa hoteli ya Sunsail, Bw Ali Bunu ambaye kwa sasa anaendeza upya ujenzi wa hoteli yake alisema kuna dalili njema ya sekta ya utalii kuimarika kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya awali.

Vijana wa Huduma za matembezi ya watalii ufuoni pia wameahidi kutoa huduma bora zaidi kwa watalii wanaozuru Lamu mwaka huu.

Wakiongozwa na Bw Salim Ali, walisema wanaendeleza mikakati kuhakikisha kuwa usafi wa fuo za bahari kote Lamu unadhibitiwa vilivyo.

“Tumejiandaa kukaribisha watalii ambao tayari wameanza kuja hapa Lamu kwa msimu wa mwezi Julai na Disemba. Tumezindua kampeni ya kusafisha fuo zetu za bahari na hata kuelimisha umma wa Lamu kuepuka kutupa ovyo taka kwenye fuo zetu. Watalii wote wanakaribishwa Lamu,” akasema Bw Ali.

Ni juma hili ambapo idara ya utalii ya Kaunti ya Lamu ilitangaza ongezeko la kiwango cha watalii wanaozuru Lamu kwa hadi asilimia 70.

You can share this post!

Fedha za wanasiasa mnazotumia kujenga makanisa ni chafu,...

‘Mchungaji’ achoma nyumba mkewe kumtomzalia...

adminleo