Bado tuko pamoja, Ruto apuuza mpasuko ndani ya Jubilee
ABDIMALIK HAJIR na LEONARD ONYANGO
NAIBU Rais William Ruto amepuzilia madai ya mgawanyiko baina yake na Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na siasa za 2022.
Bw Ruto, ambaye alikuwa akizungumza Jumapili katika eneobunge la Narok Kusini, alisema madai ya mgawanyiko ndani ya Jubilee yanaendeshwa na wale aliowataja kama ‘manabii wa uongo’ kwa nia ya kugawanya Kenya kwa misingi ya kikabila.
Kumekuwa na madai ya mgawanyiko kati ya Bw Ruto na Rais Kenyatta, ambao unaonekana kusambaa hadi katika chama cha Jubilee.
Hali hii ilianza kujitokeza baada ya Rais kuafikiana kufanya kazi na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, jambo ambalo lilionekana kumwathiri Naibu Rais hasa kuhusiana na siasa za 2022.
Majuzi Bw Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakirushiana maneno licha ya wao kuahidi hadharani kuzika tofaurti zao na kuunga mkono juhudi za kufanya kazi pamoja.
Wanasiasa kutoka ngome ya Bw Ruto ya Rift Valley pia wamekuwa wakilalamika kuwa vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi vinafanywa kwa ubaguzi.
Lakini jana Bw Ruto alisisitiza Jubilee iko imara: “Mimi sijalalamika na ninaendelea kuchapa kazi na Rais Uhuru Kenyatta amefurahishwa na kazi hiyo,” akasema Bw Ruto.
Bw Ruto, ambaye alikuwa ameandamana Narok na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, magavana Joseph ole Lenku (Kajiado) na Samuel Ole Tunai (Narok), alisema Jubilee hakikubuniwa kwa lengo la kushinda uchaguzi bali kuboresha maisha ya Wakenya.
Wengine waliokuwepo ni wabunge Lemanken Aramat (Narok Mashariki), David Ole Sangok (Maalum), Johana Ng’eno (Emurua Dikirr), Gabriel Ole Tongoyo (Narok Magharibi), Dominic Kosgey (Sotik), Joyce Korir (Mwakilishi Wanawake Bomet) na Soipan Tuya (Mwakilishi Wanawake Narok).
“Ninahimiza hao manabii wa mgawanyiko kuachana na Jubilee. Tunajua tulipotoka, tulipo saa hizi na tuendapo. Katika chama cha Jubilee tungali pamoja na lengo letu ni kuunganisha Wakenya wote na tuna mpango wa kufanikisha hayo,” akasema.
Naye Seneta Sakaja alisema Jubilee hakitatikisika: “Wale wanaodai mgawanyiko ndani ya Jubilee wamezoa siasa za kuzozana. Jubilee ni imara na kazi tuliyoanza 2013 inaendelea hadi baada ya 2022.”
Kiongozi Garissa, Kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale alisema Rais Kenyatta na Bw Ruto wangali marafiki na na wanaendeleza ajenda ya chama cha Jubilee.
“Rais anatoa mwelekeo wa chama na sisi, akiwemo Naibu Rais, tunafuata,” akasema Bw Duale.