• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Ajabu mwanamume kumea uke kwa nyeti zake baada ya kuchepuka

Ajabu mwanamume kumea uke kwa nyeti zake baada ya kuchepuka

Na STEPHEN ODUOR

KUMETOKEA kioja katika Kaunti ya Tana River, eneo la Tana Delta baada ya mwanamume mmoja kudai kumea sehemu ya siri za mwanamke kando na zake katika hali tatanishi.

Kulingana na mkewe mwathiriwa, hali hiyo ilijitokeza zaidi ya wiki moja iliyopita baada ya kunaswa kwenye fumanizi na mke wa mtu.

Alisema kwamba mumewe alikumbwa na hali hiyo baada ya kukataa sharti la mlalamishi kutaka kushirikia ngono naye, sawa na mumewe alivyomfanyia mkewe. Mlalamishi huyo alitambuliwa tu kama Joseph.

Mke wa mshukiwa pia alisema alikataa sharti hilo kama njia ya kusuluhisha mzozo huo.

“Joseph alitaka kufanya mapenzi nami kama mume wangu alivyofanya na mkewe ila sote wawili tukakataa,” akasema.

Ni baada ya mzozo huo ambapo Joseph aliondoka kitaratibu, ila akaapa kwamba lazima mtu huyo “angelipia” makosa yake.

Siku tatu baadaye, mshukiwa aligundua uvimbe fulani chini ya sehemu zake za siri, ila akaupuuzilia mbali kama hali ya kawaida.

Hata hivyo, hali ilizidi kuwa mbaya wakati alipoamua kwenda kuoga, kwani uvimbe huo uligeuka ghafla kuwa sehemu za siri za kike, jambo lililothibitishwa na mkewe.

“Alinijia akilia, akinirai nimuelezee kuhusu hali yake. Nilipochunguza vizuri, nilibaini kwamba uvimbe huo unafanana kabisa na sehemu za siri za kike,” akaelezea.

Hata hivyo, masaibu yake hayakuishia hapo kwani usiku uliofuata, waligundua kwamba alikuwa amepata hedhi, kama mwanamke wa kawaida.

Alimwamsha mumewe kuhusu kioja hicho, jambo ambalo lilimshangaza.

Tangu wakati huo, mwanamume huyo amekuwa akijificha nyumbani mwake, huku akienda hedhi kila baada ya saa tatu. Ni mkewe na wazee wachache ambao wamekuwa wakifahamu kuhusu jambo hilo la kiajabu.

Kwa upande wake, mlalamishi anadaiwa kuondoka nyumbani kwake huku mkewe akitoroka vilevile.

Juhudi za wazee kusuluhisha hali hiyo hazijazaa matunda yoyote.

Mkewe mwathiriwa amebadilisha nia na kukubali sharti la mlalamishi kulala naye, ila kulingana na wazee, Joseph sasa hamtaki.

Mzee mmoja, Hiribae Kofa, aliiambia Taifa Leo kwamba badala yake, Joseph anataka Sh300,000 “ili kumrejesha mwathiriwa katika hali ya kawaida.”

Kwa hayo, familia inawaomba wahisani kuisaidia kupata fedha hizo kwani ni vigumu kwao kuzipata kwani hawana uwezo huo.

You can share this post!

Kizaa madiwani wakilaumiana kula hongo wazime ripoti

Kibarua cha Matiang’i: Mkwaruzano na wanasiasa...

adminleo