• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Shinikizo Joho amuunge mkono Ruto 2022

Shinikizo Joho amuunge mkono Ruto 2022

BRIAN OCHARO na LUCAS BARASA

WABUNGE wa Pwani wamempa Gavana Hassan Joho changamoto aungane na Naibu Rais William Ruto, kama bado ana azimio la kuwahi kuwa rais wa Kenya.

Wabunge ambao awali walikuwa wandani wa gavana huyo wa Mombasa ambaye ametangaza nia ya kuwania urais 2022 wamekuwa wakimpigia debe Naibu Rais anayetarajia kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Mbunge wa Msambweni, Bw Sulaiman Dori, alisema haitakuwa rahisi kwa gavana huyo aliye pia Naibu Kiongozi wa Chama cha ODM kushinda urais kama hataungana na wabunge wa Pwani.

“Huwezi kutimiza azimio lako bila kushirikiana na kila mmoja wetu. Huwezi kutegemea kura za sehemu moja ya nchi kushinda urais,” akasema mbunge huyo ambaye ni mmoja wa waasi wa ODM katika eneo la Pwani.

Alikuwa akihutubu kwenye mkutano uliohudhuriwa na Bw Ruto katika eneobunge la Kisauni, Kaunti ya Mombasa.

Bw Ruto amefanya mikutano mingi ya kisiasa anayodai ni ya maendeleo Pwani katika siku za hivi majuzi, tangu Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga walipoweka muafaka wa maelewano Machi 9.

Katika chaguzi za urais zilizopita, eneo hilo lilimpigia Bw Odinga kura kwa wingi na ODM ikashinda viti vingi vya kisiasa. Bw Joho anatumai kutumia umaarufu huo wa upinzani kuwania urais 2022 atakapokamilisha hatamu yake ya pili ya ugavana.

Bw Joho alihudhuria hafla ya kuzindua awamu ya kwanza ya barabara ya Dongo Kundu iliyosimamiwa na rais, ambapo alitangaza kushirikiana na rais kimaendeleo, lakini hajahudhuria hafla yoyote kati ya nane zilizofanywa na naibu rais eneo hilo kufikia sasa.

“Muungano wa Bw Joho na Bw Ruto hauwezi kushindwa. Ni lazima gavana ashirikiane na jamii zingine ndipo ahakikishe atashinda,” akasema Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Owen Baya.

Wabunge zaidi ya kumi waliohudhuria hafla hiyo ya Jumamosi akiwemo Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, walitetea hatua yao kumuunga mkono Naibu Rais na kusema walifanya hivyo kwa manufaa ya wakazi wa Pwani.

You can share this post!

Mwalimu ajitia kitanzi na kuacha ujumbe kushauri wanaume

Wito kwa jamii ya Wakamba iitishe matangi ya maji kama...

adminleo