• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Mbona KDF wasiondolewe Somalia? ashangaa mbunge

Mbona KDF wasiondolewe Somalia? ashangaa mbunge

Na CHARLES WASONGA

HUENDA serikali ikalazimika kuwaondoa wanajeshi wake (KDF) 4,000 walioko nchini Somalia ikiwa ombi la Mbunge wa Mandera Mashariki Omar Maalim litapitishwa bungeni.

Kwenye ombi hilo ambalo lilipokelewa na afisi ya Spika Justin Muturi Jumanne, mbunge huyo anasema kuwa wakazi wa eneo bunge lake wanataka wanajeshi hao kupelekwa katika mpaka wa Kenya na Somalia

Alisema kuwa japo lengo asilia la serikali la kuwapeleka wanajeshi hao nchini Somalia lilikuwa kuhakikisha amani inadumu nchini azma hiyo haijaafikiwa.

“Tunasikitika kuwa lengo hilo halijatimizwa kwa sababu Kenya imekuwa ikishuhudia mashambulia ya kigaidi kila mara, wahusika wakuu wakisema wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab. Visa hivyo vimekithiri zaidi hata kuliko zamani,” akasema Bw Omar, akisema Wakenya wataendelea kuathiriwa na mashambulio ya kigaidi ikiwa KDF wataendelea kukaa Somalia.

Wanajeshi wa KDF walipelekwa Somalia mnamo mwaka wa 2011 chini ya mpango wa “Operation Linda Nchini” .

Lakini tangu wakati huo, kulingana na Bw Omar, Kenya imeshuhudia msururu wa mashambulio ya kigaidi yakilenga vitua vya polisi, magari ya polisi na taasisi za elimu, mikutano ya kidini na majengo ya kibiashara na kupelekea maafa na uharibifu mkubwa wa mali.

“Kwa mfano 2013 kulitokea shambulio la Wastegate ambapo watu 67 walikufa, shambulio la Mpeketoni mnamo 2014 ambapo watu 60 waliuawa kinyama, na shambulio katika Chuo Kikuu cha Garissa ambapo watu 149 waliuawa, miongoni mwao wakiwa wanafunzi 146.

Kando na hayo, wanajeshi wengi wa KDF wameuawa nchini Somalia tangu wakati huo.

Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa kumetokea mashambulio 155 ya kigaidi nchini tangu mwaka wa 2012.

Mashambulio hayo yameshuhudiwa katika kaunti za Nairobi, Garissa, Wajir na Mandera.

Omar anasema hatua ya kuwapelekea wanajeshi wa KDF nchini Somalia kuhudumu chini ya Mwavuli wa Kikosi cha Umoja wa Afrika (AMISOM) kumehatarisha hali ya usalama nchini.

“Taathira nyingine za mashambulio ya kigaidi ni kudorora kwa huduma za kiafya, elimu, uchumi na viwango vya maisha baada ya madaktari, walimu na wafanyakazi wengine wa sekta ya umma kuhama maeneo ya kaskazini mashariki mwa Kenya,” akasema Bw Omar.

Hata hivyo, serikali imeshikilia kuwa wanajeshi hao watasalia Somali hadi wakati ambapo usalama utaimarika baada ya wanajeshi wa Amisom kutokomeza kabisa wanachama wa Al Shabaab.

Ombi la Bw Omar sasa litajadiliwa rasmi bungeni wiki ujao litakapoorodheshwa na Kamati ya Bunge kuhusu Shughuli za Bunge (HBC) inayoongozwa na Spika Muturi.

Mnamo Mei mwaka huu Mbunge wa Ainabkoi William Chepkut alipendekeza kwamba mikakati ambayo imekuwa ikitumiwa na KDF kupambana na Al Shabaab ifanyiwe marekebisho.

“Hii ndio njia ya kipekee kuhakikisha kuwa wanajeshi wetu hawaendelei kuuawa kinyama nchini Somalia. Serikali inapasa kukumbatia mikakati ya kisasa ya kiusalama pamoja na vifaa ili kuwadhibiti magaidi wa Alshabaab,” akasema Bw Chepkut alishinda kiti chake kama mgombeaji huru.

You can share this post!

Madaktari wa Cuba wavutia wagonjwa hospitalini

Hamtawahi kusikia wizi tena NYS, serikali yaahidi Wakenya

adminleo