Mnikome na pesa zangu, Ruto aonya wakosoaji
Na VALENTINE OBARA
NAIBU Rais William Ruto, amepuuzilia mbali watu wanaomkashifu kwa kutoa michango mikubwa ya fedha makanisani karibu kila wikendi.
Akizungumza Jumapili alipohudhuria ibada katika Kanisa la AIPCA lililo mtaani Kayole, Kaunti ya Nairobi, Bw Ruto alitaka watu wakome kuchunguza anakotoa pesa ambazo yeye hutoa makanisani.
“Ukiwachunguza sana utakuta pesa zao huwa wanatumia usiku wakipeleka kwa waganga na wachawi. Yetu sisi tunaleta kanisani mchana kwa kazi ya Mungu,” akasema.
Viongozi kadhaa hasa wa upinzani na baadhi ya wananchi katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakitilia shaka anakotoa mamilioni ya pesa za kutoa kwa harambee karibu kila wikendi.
“Sisi huwa hatuwaulizi kuhusu pesa zao wanazopeana usiku kwa waganga na wachawi kwa hivyo pia wao waachane na sisi totoe zetu kanisani,” akasema, bila kutaja mtu yeyote.
Katika hotuba yake, alitangaza kuwa serikali imetenga Sh3 bilioni kukarabati soko la Gikomba ambalo lilichomeka hivi majuzi na kusababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali.
Wakati huo huo, aliondolea lawama afisi ya rais kuhusu vita dhidi ya ufisadi na kusema kuna asasi zilizo na mamlaka ya kupambana na janga hilo linalopotezea taifa mabilioni ya pesa.
Kulingana naye, kitengo kikuu cha utawala kinachosimamiwa na Rais Uhuru Kenyatta kina jukumu la kuendesha maendeleo ya kuboresha maisha ya mwananchi na lile la kupambana na ufisadi liko chini ya idara kama vile Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Mahakama na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
“Sisi sote tumekubaliana kwamba kazi yetu itapimwa kwa barabara, maji, stima na shule ambazo tutajenga. DCI, DPP, EACC kazi yao itapimwa kwa uchunguzi wanaofanya kuhusu uharibifu wa pesa za umma na ufisadi. Mahakama kazi yake itapimwa kwa haki itakayotendwa kuhakikisha mali ya umma iko sawasawa,” akasema.
Bw Ruto ambaye anapanga kuwania urais 2022 aliongeza kuwa serikali itahakikisha kila kitengo kinapokea mahitaji yanayohitajika kutekeleza majukumu yao akataka wote watekeleze majukumu inavyohitajika.
Sakata za ufisadi zimezidi kuibuka katika taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Kampuni ya Usambazaji Umema ya Kenya Power, ambayo maafisa wake wakuu waliopo na walioondoka walianza kukamatwa Ijumaa wiki iliyopita.
Baadhi ya wandani wa naibu rais wamekuwa wakidai kuwa juhudi hizo za kupambana na ufisadi zilizoshika kasi zinalenga washirika wa Bw Ruto kwa minajili ya kuhujumu mipango yake ya kushinda urais ifikapo 2022.
Bw Ruto alikuwa ameandamana na viongozi mbalimbali wakiwemo Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, na wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Kanini Kega (Kieni), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Charles Kanyi (Starehe), John Kiarie (Dagoreti Kusini) na George Theuri (Embakasi Magharibi).