• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Kuria akaangwa kusema Obama alitoa hotuba ya kudhalilisha Nyanza

Kuria akaangwa kusema Obama alitoa hotuba ya kudhalilisha Nyanza

NA PETER MBURU

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amejipata kubanwa na Wakenya katika mtandao wa Facebook, baada ya kuchapisha ujumbe wa kupuuzilia ziara ya Rais Mstaafu wa Marekani nchini Barack Obama kuwa haina manufaa.

Kwa kupitia ukurasa wake wa Facebook, Bw Kuria usiku wa Jumatatu alichapisha ujumbe akishangazwa na Wakenya ambao walichangamkia ziara ya Bw Obama, akisema wakati wa miaka minane ya uongozi hakufanyia Kenya na Afrika kitu cha kujivunia.

Mbunge huyo aliendelea kukashifu hatua ya Gavana wa Siaya Cornel Rasanga kudunishwa baada ya kukaguliwa na walinzi, na viongozi wa eneo hilo kwa jumla kunyimwa nafasi kupiga siasa.

“Lakini Waafrika haswa Wakenya ni watu wa kushangaza. Barack Obama alikuwa Rais wa Marekani kwa miaka minane na hakufanyia Kogelo chochote, Kenya wala Afrika. Leo hii ametembelea Kenya na tunafunga barabara zote kwa ajili yake,” akasema Bw Kuria.

“Kisha anafika Kogelo, Gavana wa eneo hilo anakaguliwa naye rafiki yangu na babake Lupita Nyong’o anafanywa shabiki,” akaendelea mbunge huyo.

Kisha kwa kutumia lugha isiyokuwa nafuu sana kutoa taswira ya Bw Obama, mbunge huyo akapuuza hotuba aliyotoa pamoja na dadake Auma Obama kuwa iliwadhalilisha viongozi wa Nyanza.

Lakini ujumbe wa mbunge huyo ulikumbana na vita vikali kutoka kwa wakenya ambao walimlaumu Bw Kuria kwa kumwingilia Bw Obama, ilhali makossa ni ya viongozi wa Kenya.

Jumbe za wakenya wengi ziliashiria kuwa matamshi ya Bw Kuria hayakuwiana nao vyema, wakiwataka viongozi wa humu nchini kusuluhisha matatizo ya taifa kwanza kama wizi wa pesa za umma kabla ya kumnyooshea kidole Rais Obama.

“Umeelekeza lawama zako mahali pabaya. Ndani ya serikali yetu, thuluthi ya pesa za umma katika bajeti zinaibiwa. Unataka atufanyie nini wakati sisi wenyewe tunaiba pesa zetu,” akasema Job Kuria.

“Obama ni muamerika si mkenya, sisi kama wakenya hatukumpigia kura, tuliwapigia wakenya wenzetu kama wewe lakini badala ya kutufanyia kazi mnatuchochea namna Obama hajatusaidia, fanyeni kazi yenu namna tulivyowapa,” akasema Joseph Wainaina.

“Alikuwa rais wa Amerika, sio Kenya. Marais wetu na viongozi wengine ndio walijishughulisha na kukama uchumi wa taifa kwa hivyo tusimlaumu Obama,” akasema Alecks Agege.

“Tuna rais ambaye tuliomchagua, hatuwezi kulalamikia aliyekuwa rais wa wengine. Hatua yake inafaa kurudishiwa shukrani ila si kukashifiwa,” akasema Joy Elisia.

You can share this post!

Wakazi wa Kogelo watamauka kuzuiwa kuhudhuria hotuba ya...

Kalameni ajuta kuwatongoza binti za mama pima

adminleo