• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Misri kunyonga watu 75 waliohusika kwa machafuko 2013

Misri kunyonga watu 75 waliohusika kwa machafuko 2013

Na MASHIRIKA

Mahakama ya Misri mnamo Jumamosi iliwahukumu watu 75 kunyongwa, wakiwemo viongozi wa kundi la Muslim Brotherhood.

Hukumu hiyo sasa imewasilisha kwa kiongozi mkuu wa kidini wa nchi hiyo. Kulingana na sheria ya Misiri, kiongozi huyo anafaa kutoa ushauri kuhusu hukumu za kifo ingawa maoni anayotoa sio ya kisheria na waliohukumiwa wana haki ya kukata rufaa.

Waliopatikana na hatia walikuwa miongoni mwa watu 713 walioshtakiwa kwa mauaji ya polisi na kuharibu mali kwenye ghasia zilizotokea nchi hiyo 2013 kati ya maafisa wa usalama na wafuasi wa Rais aliyetimuliwa Mohamed Morsi.

Viongozi wakuu wa Muslim Brotherhood, Mohamed el-Baltagui, Issam al-Aryan na Safwat Hijazi walikuwa kizimbani ilhali watu 31 walihukumiwa bila kuwepo kortini.

Aidha mwanahabari Mahmud Abu Zeid, maarufu kama Shawkan, ambaye mwezi Mei alipokea tunzo kutoka kwa shirika la Unesco ni mmoja wa walioshtakiwa. Mahakama iliahirisha uamuzi dhidi yake.

Mnamo Agosti 14 2013, moja ya siku umwagikaji mkubwa wa damu ulishuhudiwa Misri katika siku za hivi punde, baada ya jeshi kumtimua Morsi mamlakani, polisi walitumwa kuwatawanya waandamanaji eneo la Rabaa al-Adawiya jijini Cairo.

Watu wapatao 700 waliuawa katika muda wa saa chache Rabaa al-Adawiya na katika eneo la Nahda Square ambapo maandamano mengine yalifanyika.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu Amnesty International na Human Rights Watch yalisema watu 40,000 walikamatwa mwaka wa kwanza baada ya Morsi kuondolewa mamlakani.

You can share this post!

Korti yatoa mwanya kwa Museveni kutawala maisha

Kisanga polo kufumania mganga akichovya asali yake

adminleo