Spika aitisha ripoti ya wabunge waliozuru Urusi kutazama Kombe la Dunia
Na DAVID MWERE
SPIKA wa bunge la taifa, Bw Justin Muturi, amewataka wabunge waliotumia pesa za umma kwenda Urusi kutazama Kombe la Dunia waandike ripoti yao ili itathminiwe na bunge.
Agizo la Bw Muturi lilitolewa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Michezo, Tamaduni na Utalii, Bw Victor Munyaka, kukosa kuwasilisha ripoti hiyo mwezi mmoja baada ya dimba hilo kukamilika.
Imekuwa kawaida kwa wabunge kuwasilisha ripoti bungeni kila wakati wanaporejea nchini kutoka ziara za nje za kikazi.
Ripoti hiyo isipowasilishwa, itathibitishwa kuwa Wakenya hawakukosea walipokasirishwa na ziara hiyo walipoona kwamba wabunge walienda Urusi kwa starehe zao za kibinafsi.
Wakati Bw Munyaka alipoitwa na spika bungeni Ijumaa pale wenyekiti wa kamati zingine walipokuwa wakiwasilisha ripoti zao, wengi walitarajia angetumia nafasi hiyo kukosoa wale waliowakashifu kwa kutumia vibaya pesa za umma.
Lakini Mbunge huyo wa Machakos Mjini alisababisha ishukiwe ni kweli hawakwenda Urusi kikazi kwani ripoti alizowasilisha hazikuhusiana na dimba hilo.
“Bado ninasubiri ripoti kuhusu Kombe la Dunia ya Urusi kutoka kwa wanaohusika,” akasema Bw Muturi.
Bw Munyaka alionekana amenaswa bila kutarajia ikabidi ainuke kitini mwake ingawa hakutaka.
“Kamati ingali inakamilisha ripoti kuhusu Urusi. Itawasilishwa wiki mbili zijazo na ninaomba spika atoe nafasi kwa ripoti hiyo kujadiliwa kwa sababu ina umuhimu mkubwa,” akasema Bw Munyaka.
Ripoti hizo huwa muhimu kwa sababu huwa zinatumiwa kwa utengenezaji wa sera na sheria ambazo hulenga kuboresha uwezo wa Kenya katika nyanja mbalimbali.
Pia huwa zinatumiwa kutoa maelezo kwa nchi zingine ambazo hazikupata nafasi kutuma wawakilishi katika mataifa hayo ya kigeni.
Ziara ya wabunge wa Kenya nchini Urusi ilifichuka walipoeneza picha zao katika mitandao ya kijamii wakiwa wanaburudika katika viwanja vya michezo na sehemu zingine mbalimbali.
Ikizingatiwa kuwa kamati zingine zimewahi kukosa kuwasilisha ripoti zao kuhusu ziara za nje, haitakuwa jambo la kushangaza ikiwa kamati ya michezo pia itakosa kufanya hivyo.
Hata hivyo, hatari iliyopo ni kuwa hii ni ziara iliyogonga vichwa vya habari kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma na hivyo basi bunge litajipatia sifa ya kutumia mamilioni ya pesa za mlipaushuru kwa maslahi ya kibinafsi ya wabunge.
Ilisemekana wabunge karibu 20 walisafiri kwenye ziara hiyo ambayo ilighadhabisha wengi.
Wabunge waliohojiwa na wanahabari wakati huo walijitetea na kusema kwamba hiyo ilikuwa mojawapo ya majukumu yao, na wengine wakadai walijifadhili wenyewe.
Baadhi ya waliokasirishwa na jinsi mamilioni yalivyotumiwa kwa ziara hiyo walishangaa kwa nini serikali haingefadhili wachezaji wa timu ya taifa kwenda Urusi badala ya kuwalipia wabunge.