• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Agizo la HELB laibua hofu katika Chuo Kikuu cha Moi

Agizo la HELB laibua hofu katika Chuo Kikuu cha Moi

Na DENNIS LUBANGA

CHUO Kikuu cha Moi kimejipata katika njiapanda baada ya Halmashauri ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) kuwaagiza wanafunzi wake wa mwaka wa nne kuanza kulipa mikopo yao.

Wanafunzi hao, ambao wamekaa sana chuoni humo kutokana na changamoto za malazi, wamesema kwamba hawapaswi kuadhibiwa kutokana na kutowajibika kwa taasisi hiyo.

Wakiongozwa na Bw Ochieng’ Obunga, wanafunzi hao walisema kuwa halmashauri hiyo ilikuwa imetishia “kuwachukulia hatua” ikiwa hawangeanza kulipa mikopo yao kuanzia mwezi huu.

“Mbona tunaadhibiwa kwa makosa ambayo hatujayafanya? Bado hatuna uwezo wa kuanza kulipa mikopo hiyo kwani tungali shuleni,” akasema Bw Obunga.

Mnamo Julai 27, halmashauri hiyo iliwatumia arafa kwao kuwaonya kwamba itakuwa ikiwatoza faini ya Sh5,000 kila mwezi, kwani muda rasmi wa kuanza kulipa mikopo hiyo ulikuwa umeisha.

“Hamjambo. Muda wa kuanza kulipa mkopo wako umeisha. Ili kuepuka faini ya Sh5, 000 kila mwezi, tafadhali anza kulipa mkopo wako,” ikaeleza arafa hiyo.

Wanafunzi hao wenye ghadhabu wanadai kwamba wamekuwa wakikishinikiza chuo hicho kuiambia halmashauri kuhusu masaibu yao. Wanasema kuwa si haki kwao kupigwa faini ikizingatiwa bado hawajamaliza masomo yao kirasmi.

“Tumekaa shuleni sana kutokana na changamoto za kupata malazi na mgomo wa wahadhiri. Mbona usimamizi wa chuo hauwezi kufafanua hili kwa HELB?” akashangaa Obunga.

Akaongeza: “Ikizingatiwa kwamba lazima tulipe mikopo hii, hatupaswi kuhangaishwa Halmashauri inapaswa kuelewa matatizo yetu.”

Lakini kwenye barua kwa wanafunzi hao mnamo Julai 16, Msimamizi Mkuu wa Masuala ya Wanafunzi Prof Nathan Ogechi alisema kwamba Naibu Chansela wa Chuo amemwandikia Afisa Mkuu Mtendaji wa HELB Charles Ringera kuhusu matatizo hayo. Aliiomba halmashauri kutowatoza faini wanafunzi hao hadi pale watakapomaliza rasmi masomo yao.

Halmashauri hiyo ilijibu kwa kusema imepokea barua kutoka kwa chuo hicho: “Kwa niaba ya Naibu Chansela, nilipokea barua nambari HELB/RD /39/006/11. Tutashauriana na kutekeleza agizo hilo.”

Kwa sasa, wanafunzi hao wanautaka usimamizi wa chuo kujitokeza wazi kuelezea kinachoendelea.

Vile vile, wametishia kufika kwa Wizara ya Elimu ili kuishinikiza kuingilia kati.

“Chuo hiki kimechelewesha mipango yetu ya kumaliza masomo kwa muda uliowekwa. Hili ni suala nzito, ambalo utatuzi wake umeonekana kukishinda,” akasema.

Akaongeza: “Ikiwa ni hivi, basi Wizara ya Elimu inapaswa kuingilia kati ili kutusaidia.”

You can share this post!

Spika aitisha ripoti ya wabunge waliozuru Urusi kutazama...

Aisha Jumwa alazwa kwa mshtuko wa kulaki mwili wa kaka yake

adminleo