Habari Mseto

Afisa wa KDF jela miaka 20 kwa kunajisi watoto wawili

August 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Titus Ominde

MWANAJESHI mstaafu, 59, ambaye alipatikana na hatia ya kunajisi watoto wawili wasichana wa umri wa miaka 11 na 12 mtawalia alifungwa jela miaka 20 na mahakama moja mjini Eldoret.

Maelezo ya mashtaka yalisema kuwa Rashid Wanyama Omar alinajisi mtoto wa umri wa miaka 12 mnamo Oktoba 11 mwaka wa 2015 katika eneo la Sirikwa Quarry Eldoret West kaunti ya Uasin Gishu.

Mshtakiwa huyo alikabiliwa na shtaka jingine la kunajisi mtoto mwingine wa umri wa miaka 11 ambapo alitumia vidole kumdhulumu mlalamishi kimapenzi tarehe sawia.

Walalamishi hao ambao waliambia mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa mtu ambaye walimfahamu vyema aliwaita nyumbani mwake ambapo aliwanajisi baada ya kuwashawishi kutizama filamu ya ngono pamoja.

Katika taarifa za ushahidi dhidi ya mshtakiwa, waliambia mahakama kuwa mshtakiwa alimbeba msichana wa umri wa miaka 12 hadi kitandani mwake ambapo alimnajisi.

Mtoto mwingine wa miaka 11 aliambia mahakama kuwa mshtakiwa alimdhulumu kimapenzi kwa kutumia vidole.

Ushahidi uliotolewa na walalamishi upande wa mashtaka ulizingatia kwa kina uchunguzi wa matibabu ambao ulitolewa na daktari kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi ambao ulithibitisha kuwa walalamishi walinajisiwa.

Akitoa hukumu hiyo hapo jana, hakimu mkazi wa Eldoret alisema ushahidi ambao uliwasilishwa mahakamani humo ulibaini kuwa mshtakiwa alikuwa na hatia.

“Baada ya kuchunguza kwa kina ushahidi uliowasilishwa mahakamani na upande wa mashtaka, mahakama hii imethibitisha bila kusita ya kwamba ulitekeleza makosa ya unajisi kinyume na sheria ya watoto ya mwaka 2006,” alisema hakimu Emily Kigen.

Bi Kigen alimfunga mshtakiwa kwa miaka 20 gerezani.

Hata hivyo mahakama ilimpa siku 14 kukata rufaa iwapo hakuridhsihwa na uamuzi husika.