Habari Mseto

UBOMIAJI: Sonko na Waititu warukiana mitandaoni

August 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA PETER MBURU

Semi za Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu za kukosoa ubomoaji wa majumba yaliyojengwa karibu na mito na badala yake akipendekeza mikondo ya maji ibadilishwe zimezidi kuibua hisia mseto kote nchini, huku baadhi ya viongozi wakiingilia.

Gavana wa Nairobi Gideon Mbuvi ‘Sonko’ alimvamia Bw Waititu kutokana na pendekezo hilo, akimlaumu kuwa hayaelewi masuala ya mazingira na amenyakua ardhi za umma ambazo anahofia zitatwaliwa.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Gavana Sonko alimkaripia mwenzake wa Kiambu, akimjulisha kuwa majengo mengine yote yaliyoko katika mashamba ya umma ama yanayohatarisha mazingira hayatasazwa.

“Rafiki yangu ashughulike na kaunti yake. Anafaa kujua hatuchanganyi urafiki na kazi. Hata (hoteli ya) Weston, ploti yangu ya Buruburu Casurina cocobeach, Taj Mall na majengo mengine hayatasazwa yakipatkana kuwa katika shamba la umma ama karibu na maeneo ya maji,” akasema Bw Sonko.

Gavana huyo alizidi kuibua madai kuwa Bw Waititu ana kituo cha mafuta ambacho kiko katika shamba la umma, akirejelea machapisho ya habari ya siku za mbeleni ambayo gavana huyo wa Kiambu amewahi kuhusishwa na unyakuzi wa ardhi.

“Kwanza anafaa kutueleza kuhusu hali ya kituo cha petrol kilichojengwa katika shamba la unyakuzi la kuelekea makutano ya barabara ya Mihango na Njiru,” akasema Bw Sonko.

Hata hivyo, katika mahojiano na kituo cha Milele fm, Gavana Waititu jana alizidi kushikilia msimamo wake kuwa wazo lake la mito kuundiwa mikondo mipya badala ya majengo yaliyogharimu pesa nyingi kubomolewa ni jambo ambalo linawezekana.

“Tunawezajenga kuta kupea mto mkondo mpya, haina shida inawezekana kusongeza mto. Kuna hesabu nyingi na lazima watu wasikizwe, mimi ni mtu ambaye nimewekeza katika sekta ya ujenzi kwa miaka mingi na hiyo ni ukweli, kabla ukashifu mtu msikize, muulize maswali na kuna habari nyingi (atakupa) na lazima watu wajieleze ndio ijulikane,” akasema Bw Waititu.