• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Mitandao ya kijamii itasaidia wanyonge kupata haki lakini kwa kufuata kanuni hizi

Mitandao ya kijamii itasaidia wanyonge kupata haki lakini kwa kufuata kanuni hizi

NA FAUSTINE NGILA

MTINDO ambapo asasi zinazotegemewa kutenda haki katika visa mbalimbali vya uhalifu hutegemea mitandao ya kijamii, umeibua hisia mseto kutoka kwa wataalamu wa masuala ya haki na teknolojia.

Katika mwezi huu wa Agosti, mitandao ya kijamii imewasaidia pakubwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji na mwenzake wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Bw George Kinoti katika juhudi zao za kukomesha maovu kwa jamii hasa dhuluma za kimapenzi.

Ingawa kuna kanuni za mahakama kuhusu utumizi wa picha na video kama ushahidi dhidi ya mshtakiwa, imebainika kuwa iwapo mtuhumiwa atakiri mashtaka basi kanuni hizo huwa hazifuatwi.

Kulingana na wakili maarufu Cliff Ombeta, picha na video kutoka mitandaoni huwa zinafaa kuthibitishwa na mahakama kabla ya kesi kuanza, iwapo mtuhumiwa amekana mashtaka dhidi yake.

“Aliyeirekodi video au kupiga picha anafaa kujitokeza na kuandikisha taarifa kwamba ni yeye alifanya hivyo iwapo itatumika kama ushahidi halali kwenye kesi dhidi ya mtuhumiwa,” anasema.

Katika taifa ambalo asilimia 60 ya watu wote wanamiliki simu za kisasa almaarufu smartphones, unahitaji tu kutuma picha moja na itaweza kufikia Wakenya zaidi ya milioni 10.

Kenya inaongoza katika trafiki ya intaneti duniani, baada ya kuipiku Nigeria, kutokana na bei nafuu ya simu za kisasa na pia bei ya intaneti. Wakenya pia ni wapenzi wa teknolojia, na hupenda kusaka habari sana kwenye mitandao.

Ni uwezo huu wa kiteknolojia miongoni mwa wananchi ambao sasa umechangia baadhi ya waovu kuadhibiwa vikali baada ya vitendo vyao vya kishetani kurekodiwa na hatimaye kufikia ofisi za DPP na DCI na washukiwa kukamatwa na kushtakiwa mahakamani.

Kwa kuwa video huonyesha sura, eneo, mavazi na sauti ya mtu, hiyo huwa ni ushahidi usioweza kutiliwa shaka na wengi wa washukiwa hukubali walitenda uovu unaoonekana kwenye video.

Msomi wa masuala ya teknolojia na biashara aliye pia mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Dkt Bitange Ndemo, alisema ingawa teknolojia inasaidia katika juhudi za utekelezaji wa haki, ni muhimu kuwa picha, video au sauti zinazotegemewa mahakamani zithibitishwe kuwa za kweli iwapo zitatumika kama ushahidi.

Hii ni kutokana na kuwa teknolojia hiyo hiyo inaweza kutumiwa na matapeli wenye nia mbaya kuwekea watu wasio na hatia mashtaka ya uongo.

“Masuala ya mitandao ya kijamii hayafai kuaminiwa bila ithibati. Wakati mwingine watu hutumia programu ya Photoshop na kuhariri picha na video ili kusukumia mtuhumiwa lawama. Hali hii huvunja maisha ya mshukiwa kwa kumharibia sifa,” anasema.

Dkt Ndemo alieleza kuna uwezekano kuwa katika siku za usoni, mtindo wa watu kusambaza video, sauti na picha za watu waliovunja sheria utapata umaarufu zaidi, na huenda watu zaidi wakafikishwa mahakamani.

Alipendekeza kuwe na sera na sheria za kudhibiti zaidi mitandao ya kijamii.

Kwa mfano, kupitia kwa video ilizoyambazwa kwenye mitandao ya WhatsApp, Facebook, Twitter na Instagram, mwanamume mmoja kutoka Kaunti ya Makueni alijipata taabani kwa kumtwanga mkewe bila huruma.

Mwanamume huyo, Daudi Nzomo, aliyenaswa kwenye video akimpiga mke wake, Winfred Mwende, kwa ngumi na mateke, alikiri mashataka na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.

Kwenye video hiyo, Bw Nzomo, 36, anaonekana mwenye ghadhabu huku akimwadhibu mkewe kinyama licha ya watu waliokuwa karibu kumsihi amwache.

Ni kutokana na ukatili wa Bw Nzomo kudinda kukoma kumcharaza mkewe ambapo mmoja wa waliokuwa wakitazama waliamua kumrekodi akitenda uovu huo kisha akasambaza video hiyo kwa mitandao angalau aone itaweza kufikia maafisa husika na hatimaye haki kutendeka.

Wiki iliyopita, video nyingine ilichipuka kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mwanamke akimpiga mwanamume nje ya jengo moja katika barabara moja katika eneo lisilojulikana.

Mwanamke huyo anaonekana akimnyeshea mwanamume huyo ngumi na mateke huku akidai deni lake la Sh200. Mwanamume naye anasikika akilia aongezewe muda wa kulipa deni lakini ombi lake linaangukia masikio yaliyotiwa nta.

Kupitia kwa akaunti yake ya Twitter, Bw Haji alisema kuwa anamtafuta mwanamke huyo, akitaka habari kumhusu, jina lake, eneo alilomwadhibia mwanamume na siku alilotekeleza uovu huo.

Na majuzi picha ya mwanamke mwingine Bi Valarie Masibo, 29 wa mtaa wa Kipkaren, Eldoret ilisambaa mitandaoni ikionyesha akiuguza majeraha ya usoni, kwenye masikio na meno, akidaiwa kupigwa na mumewe Bw Naftali Luzeli wa miaka 26.

Ilidaiwa mama huyo alikuwa mjamzito na mumewe alimcharaza kwa kumcheleweshea chakula cha jioni.

Polisi walimkamata mshukiwa na kumzuilia katika kituo cha Yamumbi baada ya picha ya mkewe kuenea kotekote na kuzua kero mitandaoni.

Kulingana na wakili Cliff Ombeta, taarifa ikiwasilishwa mahakamani pamoja na picha au video huwa zinafaa kukaguliwa na mchanganuzi wa serikali ambaye ataidhinisha kutumika kwake kama ithibati kwenye kesi.

Mchanganuzi na mtu aliyerekodi video au kupiga picha hupewa cheti cha kuonyesha ushahidi ni halali.

“Mtaalamu wa serikali hukagua ile taarifa kisha kuilinganisha na picha au video kuhakikisha hakuna jambo lililobadilishwa. Ikiwa ni taarifa ya kweli, basi huwasilishwa mahakamani kama ushahidi,” anafafanua wakili huyo.

You can share this post!

Raila atakuwa debeni 2022 – Orengo

BLOCKCHAIN: Suluhu tosha kuzima ufisadi na wizi wa kura

adminleo