Habari za Kitaifa

Afadhali Ruto kuliko Gachagua, Oburu aambia wanaosema ‘Ruto must go’

Na VICTOR RABALLA July 15th, 2024 2 min read

SENETA wa Siaya Dkt Oburu Oginga sasa anasema kuwa wito unaoendelea wa kumbandua Rais William Ruto mamlakani huenda utaibua mtanzuko wa kikatiba na kufanya taifa likose udhabiti wa kisiasa.

Dkt Oginga, amesema maandamano yaliyoanza kupinga Mswada wa Fedha 2024 sasa yamechukua mwelekeo mpya na yanatishia demokrasia ya nchi.

Dkt Oginga ameseme kikatiba iwapo Rais  Ruto atajiondoa mamlakani, basi Naibu wake Rigathi Gachagua ndiye atachukua usukani. Hata hivyo, alimtaja Bw Gachagua kama kiongozi mbaya zaidi akilinganishwa na Rais Ruto.

“Japo wote ni viongozi wabaya, Gachagua ni mbaya zaidi, mkabila na tayari alishatangaza kuwa nchi inaongozwa kwa kutegemea mchango wa kura wa kila jamii katika uchaguzi mkuu uliopita,” akasema Dkt Oginga.

Seneta huyo ambaye ni nduguye Kinara wa Upinzani Raila Odinga, alisema Wakenya watakuwa wakijitia kitanzi zaidi wakikubali Bw Gachagua kuwa kiongozi wa nchini.

“Hata watu wakimlaumu Rais Ruto, Bw Gachagua ndiye amesababisha uteuzi uendee jamii mbili kutokana na tamaa na shinikizo ambazo amekuwa akiwekea Rais,” akaongeza Dkt Oginga.

Kwa mujibu wa Dkt Oginga, 80,  Kenya kwa sasa ipo katika njia panda na kile ambacho kinastahili kukumbatiwa ni mazungumzo ili nchi isonge mbele. Aidha seneta huyo alisema Kenya huenda ikasimamiwa na jeshi iwapo Gen Z watasababisha serikali yote iondoke mamlakani.

Gabon, Misri, Chad, Guinea, Gabon, Sudan na Niger ni kati nchi ambazo Dkt Oginga alisema zimeishia kupoteza demokrasia na kuongozwa kidikteta baada ya wananchi kuondoa tawala zilizokuwepo.

Kuzuia Kenya kuelekea njia hiyo, Dkt Oginga aliwataka wanasiasa wote watoe mwelekeo badala ya kuyatumia maandamano ya Gen Z kujinufaisha kisiasa.

“Mwelekeo ndio muhimu na wanaoyatumia maandamano hayo kujaribu kujikweza kisiasa si viongozi wazuri,” akasema mbunge huyo wa zamani wa Bondo.

Seneta huyo alisema ODM ipo tayari kwa mazungumzo na inaunga mkono kauli ya Rais William Ruto kuwa atabuni muungano ambao unahusisha wanasiasa kutoka mirengo mbalimbali ikiwemo upinzani.

Dkt Oginga, anasema wanasiasa wa upinzani kujiunga na serikali kutasaidia wao kutekeleza baadhi ya sera muhimu ambazo nao waliwaahidi Wakenya kuelekea uchaguzi wa 2022.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa hataketi tu na kutazama nchi ikielekea pabaya na badala yake atahakikisha nchi inasalia dhabiti kwa muda wa miaka mitatu iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa.

“Tunajaribu kuwaleta pamoja wanachama wa Azimio kuhakikisha kuwa kuna umoja wa nchi,” akasema.

Mwakilishi huyo wa wakazi wa Siaya kwenye seneti  aliwataka vijana washiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa 2027 na kuwachagua viongozi bora ambao watatimiza matakwa yao.