Michezo

Arteta: Sihitaji kununua mshambulizi Januari hii, Arsenal iko sawa

January 1st, 2024 3 min read

Na MASHIRIKA

KUSUASUA kwa Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kunatarajiwa kumzidishia Mikel Arteta presha ya kusajili mvamizi wa haiba kubwa mwezi huu licha ya kocha huyo raia wa Uhispania kusisitiza kuwa kikosi chake hakihitaji mchezaji yeyote mpya kwa sasa.

Fulham waliendeleza masaibu ya Gunners ligini kwa kuwapokeza kichapo cha 2-1 ugani Craven Cottage, Jumapili. Pambano hilo lilikuwa la pili mfululizo kwa vijana hao wa Arteta kupoteza. Walishuka dimbani baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool na kukubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa West Ham United katika michuano miwili ya awali.

Ni matokeo yaliyowateremsha hadi nafasi ya nne kwa alama 40, moja pekee mbele ya nambari tano Tottenham Hotspur waliokomoa Bournemouth 3-1. Ushindi wa Spurs uliendeleza vita vikali vya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao huku Arsenal sasa wakikodolea macho hatari ya kutupwa nje ya mduara wa nne-bora kwenye jedwali la EPL.

“Itatulazimu kufanya tulichofaulu kufanya katika mechi 19 za kwanza ligini msimu huu tukitegemea wachezaji wale wale walioko kikosini,” akasema Arteta.

Licha ya kutoa kauli hiyo, presha ya kuimarisha makali ya Arsenal na kusalia miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la EPL inatarajiwa kusukuma Arteta sokoni mwezi huu kusaka fowadi mzoefu atakayeweka hai ndoto za mashabiki wao. Kati ya mafowadi tegemeo wanaohusishwa pakubwa na miaba hao ni Ivan Toney wa Brentford, Victor Osimhen na Dominic Solanke ambaye tayari amefungia Bournemouth mabao 12 katika EPL msimu huu.

Hata hivyo, huenda Toney akahitaji muda zaidi kurejea katika ubora wake ikizingatiwa kwamba hajawahi kutandaza boli tangu Mei alipopigwa marafuku kwa kukiuka kanuni zinazodhibiti mchezo wa kamari miongoni mwa wanasoka.

Osimhen naye ataweka Arsenal katika ulazima wa kuvunja benki ndipo aachiliwe na Napoli waliomshawishi kurefusha mkataba wake kwa miaka mitatu zaidi majuzi. Isitoshe, huenda nyota huyo asiwe wa msaada kwa Arsenal hadi Februari baada ya kutiwa katika kikosi kitakachowajibishwa na Nigeria kwenye fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast.

Mechi dhidi ya Fulham ilikuwa ya kwanza baada ya michuano 48 tangu Januari 2022 kwa Arsenal kupoteza baada ya kufunga bao la kwanza.

“Haiwezekani tuendelee kupoteza mechi ambazo kila mtu anatarajia tushinde. Pambano dhidi ya Fulham ndilo bovu zaidi kuwahi kupigwa na Arsenal msimu huu,” akatanguliza Arteta.

“Matokeo ya mechi mbili zilizopita yanasikitisha na timu haichezi kama iliyo na ari ya kushinda ligi. Hali si shwari na wachezaji hawajitumi tena jinsi inavyotarajiwa na mashabiki. Hofu ni kuwa pengo la alama kati yetu na viongozi linazidi kuongezeka. Uthabiti wa kikosi umeshuka na ratiba ijayo ni ngumu,” akaongezea.

“Iwapo maazimio ni kurejesha hadhi ya kikosi na kushinda ufalme wa EPL, hizi ni mechi ambazo ni muhimu tuzitamalaki. Vinginevyo, mashabiki wataanza kumtia kocha presha na madhara yatakuwa makubwa zaidi. Tutajisaka upya kuwajibika ipasavyo,” akasema kiungo Declan Rice.

Kati ya klabu tano za kwanza kileleni mwa jedwali la EPL kwa sasa, Arsenal ndio wamefunga mabao machache zaidi (37). Kufikia wakati kama huu msimu jana, walikuwa wametikisa nyavu za wapinzani mara 45 huku wakijivunia alama 50 baada ya kushinda mechi 16 kati ya 20.

Mnamo Jumapili, Arteta alimweka Gabriel Jesus benchi na kupanga Eddie Nketiah katika kikosi cha kwanza licha ya fowadi huyo raia wa Uingereza kutofunga bao lolote la EPL ugenini mwaka wote wa 2023.

Idara ya ulinzi ya Arsenal pia haiko imara ikizingatiwa kwamba kikosi hicho hakijafungwa bao katika mechi moja pekee kati ya saba za Desemba 2023. Baada ya kualika Liverpool kwa raundi ya tatu ya Kombe la FA ugani Emirates wikendi hii, Arsenal watarejelea kampeni za EPL msimu kwa kumenyana na Crystal Palace mnamo Januari 20. Huenda wasiwe popote karibu na mduara wa nne-bora jedwalini wakati huo.

Leo itakuwa zamu ya nambari sita West Ham United kualika Brighton ugani London Stadium. West Ham wamejizolea alama 33 kutokana na mechi 19 zilizopiga ligini na pengo la pointi tatu linawatenganisha na Brighton wanaofunga orodha ya nane-bora.

RATIBA YA EPL (LEO JUMATATU):

West Ham vs Brighton (10:30pm)