Michezo

Asanteni sana na kwaherini, Southgate ajiuzulu baada ya kichapo fainali za Euro 2024

Na MASHIRIKA July 16th, 2024 1 min read

LONDON, Uingereza

BAADA ya kushindwa na Uhispania kwenye fainali ya Euro 2024, kocha Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza ameamua kujiuzulu wadhifa wake.

Timu hiyo maarufu kama The Three Lions ilichapwa 2-1 na Uhispania katika fainali hiyo iliyochezewa jijini Berlin, Jumapili.

Mlinzi huyo wa zamani wa klabu ya Chelsea mwenye umri wa miaka 53, amefunganya virago baada ya kuwa kwenye usukani kwa kipindi cha miaka minane tangu 2016, akichukua nafasi ya mkongwe Sam Allardyce aliyejiondoa ghafla.

Kocha huyo ambaye ameongoza timu ya taifa katika mechi 102 akiwa katika usukani alisema, “kama Mwingereza halisi, najivunia kupewa heshima kuchezea timu ya taifa na baadaye kuinoa. Kwa hakika ni heshima kubwa maishani mwangu.”

“Nitakumbuka milele nafasi hii, huku nikiamini nilijitolea niwezavyo. Lakini kila kitu kina mwisho. Sasa ni wakati wa kuanza ukurasa mpya,” aliongeza.

Southgate, ndiye kocha wa kwanza kufikisha timu ya taifa katika fainali ya mashindano makubwa tangu Sir Alf Ramsey afanye hivyo 1966.

Ameongoza Uingereza katika mashindano makubwa manne, akiisaidia kutinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 na robo-fainali mnamo 2022.

Baadhi ya mashabiki walimfokea na kumrushia chupa za plastiki timu hiyo ilipotoka sare 0-0 na Slovenia kwenye mechi ya makundi wakati wa Euro 2024.

“Kikosi tulichopeleka Ujerumani kilikuwa kizuri, lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kutwaa ubingwa. Natarajia timu hii kufanya makubwa zaidi siku za usoni. Nimeondoka, lakini nitazidi kuwa shabiki mkubwa wa timu ya taifa. Asanteni sana, kwa kila kitu.”