Habari za Kaunti

Bamburi Cement yatoa hakikisho la kuzuia mavumbi kufikia wakazi

January 11th, 2024 2 min read

NA FARHIYA HUSSEIN

BAADA ya Kaunti ya Mombasa kufunga machimbo ya Bamburi Cement kutokana na malalamishi ya wakazi wa Kwa Bulo na Bamburi, sasa kampuni hiyo imesema itashirikiana na kamati maalum na wadau muhimu ikiwemo jamii ili kuimarisha hali.

Walalamishi walisema uhifadhi wa makaa hayo unasababisha hatari za kiafya ndani ya umbali wa kilomita tatu.

Kiwanda hicho kilikuwa kimeagiza zaidi ya tani 50,000 za makaa ya mawe kupitia bandari ya Mombasa na kuanza kuhamishia kiwandani mnamo Januari 3, 2024.

Licha ya kuhamisha zaidi ya tani 40,000 za makaa ya mawe hadi eneo la kiwanda, kaunti hiyo iliikosoa kampuni hiyo kwa jinsi ambavyo inahifadhi makaa hayo kizembe katika eneo la wazi.

Wakati wa ziara ya kushtukiza ya Naibu Gavana wa Kaunti ya Mombasa Francis Thoya na afisa wa mazingira, wasiwasi uliibuka huku wafanyakazi wanaoshughulikia makaa hayo wakiwa bila vifaa maalum vya kujikinga wasipate madhara.

Ukaguzi ukiendelea eneo ambapo shughuli za kuchambua makaa ya mawe ya kampuni ya saruji ya Bamburi Cement hufanyika. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

Maafisa wa kiwanda hicho walikiri kutokuwa na leseni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira lakini walidai kuchukua tahadhari muhimu.

Kaunti hata hivyo ilielezea kutoridhishwa kwa sababu “kampuni ilipuuza ilani iliyotolewa na kaunti hapo awali”.

Kufungwa kwa shughuli za kiwanda cha makaa ya mawe kutokana na masuala ya uhifadhi kunaweza kusababisha hasara kubwa ya kifedha kwa Bamburi Cement.

Kusitishwa huko kukiendelea kwa muda mrefu pia huenda kukasimamisha uzalishaji wa saruji kwani makaa ya mawe ni kiungo muhimu katika mchakato huo.

Kampuni ya Bamburi Cement baadaye ilitoa taarifa ya kutetea ahadi yake ya uhifadhi wa mazingira lakini ikakubali “tukio la kipekee” la utoaji wa vumbi unaosababishwa na upepo wakati wa kushughulikia makaa ya mawe.

Wasimamizi walihakikisha kwamba hatua zipo ili kupunguza matukio kama haya na kusisitiza kufuata kanuni za mazingira.

Naibu Gavana Thoya, aliyeathiriwa na vumbi kutokana na kuishi karibu, alielezea kutamaushwa na utendakazi wa kampuni hiyo licha ya sura zao za nje.

Aliangazia athari za kibinafsi kama vile mtoto wake kupata pumu.

Kampuni hiyo kwa upande wake imesema kamati imebuniwa na watafanya ushirikiano na mamlaka na jamii ili kuzuia matukio kama hayo.

“Hatua hizi hazijaathiri operesheni zetu za kila siku,” imesema Bamburi Cement kwenye tangazo ambalo limechapishwa katika ukurasa wa sita wa Daily Nation toleo la Januari 11, 2024.