Habari Mseto

Changamoto za mapaparazzi katika miji mikuu nchini

January 21st, 2024 2 min read

NA RICHARD MAOSI

WAPIGAPICHA za barabarani almaarufu Street Shoots, wamesema katika kazi yao wanapitia changamoto tele, zikiwa ni pamoja na kuhangaishwa na baadhi ya maafisa wa idara za ulinzi mijini na wakati mwingine wezi wa kamera.

Jijini Nairobi biashara za kuwaingizia mapaparazzi pesa hunoga katika maeneo ya Kenyatta Avenue, Kimathi Street, Muindi Mbingu na Koinange Street.

Taifa Leo ilizungumza na mpigaji picha maarufu ambaye anajitambulisha kwa jina la utani Moss the Boss.

Moss alisema siku za wikendi wakati ambapo idadi ya wateja katikati mwa jiji kuu la Nairobi huwa kubwa, wanahangaishwa na baadhi ya watu wanaodai ni maafisa wa idara ya ulinzi.

Alisema huwa wanataka kumegewa kiasi kidogo kama hongo la sivyo wahangaishwe.

Moss alisema kwamba alisomea Uanahabari katika chuo kimojawapo jijini Nairobi, lakini akaamua kugeukia kazi ya upaparazzi baada ya kukosa ajira.

Lakini afisa mmoja wa idara ya ulinzi jijini ambaye aliomba tusichapishe jina lake, alisema baadhi ya wapigapicha wamekuwa wakichangamana na wezi wa simu.

Afisa huyo alisema kukusanyika kwa watu wengi katika eneo moja kwa kisingizio cha upigaji picha, hufanya wezi kujipenyeza hapo kuiba kutoka kwa umma.

“Biashara yenyewe inafaa kudhibitiwa kwa sababu baadhi ya wapigapicha hupiga kwenye makazi ya kibinafsi ya watu, bila hata kuomba idhini,” akasema afisa huyo.

Katika Kaunti ya Nakuru mpigajipicha mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina moja, Joseph, alisema alivamiwa na wezi wanaotumia pikipiki alipokuwa akipiga picha katika eneo la Milimani.

Wezi hao ambao wanaaminika kutoka mtaa wa mabanda wa Bondeni, walimzingira akiendelea kuwahudumia wateja na kutoa kisu wakaanza kumtishia.

Ilibidi Joseph kusalimisha kamera yake kisha wezi hao wakatoweka kwa kutumia pikipiki ambayo haikuwa na nambari za usajili.

Kamera ya mpigapicha. PICHA | RICHARD MAOSI

Joseph alisema kuwa baadhi ya wahalifu huwa wanajifanya kuwa ni wateja.

Alitoa pendekezo wapigapicha watengewe sehemu maalum za kupigia picha badala ya vichochoroni, ambapo ni rahisi kuvamiwa na kuibiwa.

Sheria inakataza kupiga picha katika baadhi ya sehemu kama vile kambi rasmi za wanajeshi, mbuga za wanyamapori au sehemu za kuhifadhi wanyama bila mpigapicha kuwa na cheti au kibali maalum.