Cheche ataka Starlets kuboresha mashambulizi
Kocha wa timu ya taifa ya vichuna walio chini ya umri wa miaka 17, Junior Starlets, Mildred Cheche, amewataka wachezaji wake kuboresha mashambulizi wa nafasi za kufunga mabao kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la kwa wanawake walio chini ya umri huo nchini Morocco kesho.
Mashindano hayo yatakamilika Novemba 7, huku timu 24 zikishiriki kuwania taji hilo la dunia. Kenya inashiriki kwa mara ya pili baada ya kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2024.
Starlets iliwasili Morocco Oktoba 8 na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Raja Casablanca Women Jumatatu wiki hii na Ghana kujiandaa kwa mashindano hayo.
Kenya ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ghana Jumatano katika uwanja wa Complexe Sportif Moulay Rachid, Casablanca, katika mechi ambayo ilifichua udhaifu wa timu hiyo katika kutumia nafasi za kufunga.
Cheche alisema mechi hizo za kirafiki zimeisaidia benchi ya kiufundi kutambua maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi kabla ya mechi yao ya kwanza ya Kundi E dhidi ya China Oktoba 19.
“Wasichana walifanya vizuri. Mechi ya kwanza haikuwa na ushindani mkubwa, lakini dhidi ya Ghana ushindani ulikuwa mkali na tuliweza kuona maeneo tunayohitaji kuboresha,” alisema Cheche.
“Tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tukashindwa kuzitumia. Lazima tufanyie kazi mashambulizi kwa sababu hilo ndilo lililotuangusha katika mechi hiyo.”
Kocha huyo pia amewataka wachezaji wake kuwa na mtazamo wa ushindi, akisisitiza kuwa wanapaswa kushiriki mashindano ya mwaka huu wakiwa na dhamira tofauti na ile ya mwaka 2024.
“Lengo si kushiriki tu, bali kushindana. Mwaka 2024 tulishiriki, lakini mwaka 2026 tunahitaji kushindana. Hii ni mara yetu ya pili, kwa hivyo wachezaji wanapaswa kuwa na mtazamo tofauti na kuamini wanaweza kushinda mechi,” alisema.
Cheche anaamini kikosi chake kiko tayari, lakini amesema benchi ya kiufundi inaendelea kuwaimarisha wachezaji kisaikolojia ili waweze kukabiliana na presha na kuzoea haraka changamoto za wapinzani wao.
Kenya ilikuwa imepanga kwenda Uhispania kwa kambi ya maandalizi kabla ya mashindano, lakini safari hiyo ikasitishwa kutokana na changamoto ya visa.
Baada ya kukabiliana na China Oktoba 19, Starlets itamenyana na Marekani Oktoba 22 kabla ya kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Samoa Oktoba 25. Mechi zote zitachezwa katika akademia ya soka ya Mohammed VI mjini Salé, Morocco.