Dimba

Compyuta yabashiri Arsenal na Man U hawatashinda ligi kuu katika msimu mpya unaoanza

Na GEOFFREY ANENE July 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

UKISALIA mwezi mmoja kabla ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ya msimu 2024-2025 ianze Agosti 16, kompyuta maalum imebashiri kuwa Arsenal na Manchester United hawatashinda ligi hiyo ya klabu 20.

Wanabunduki wa Arsenal kwa sasa wanajiandaa kwa kampeni mpya watakayoanza dhidi ya Wolves mnamo Agosti 17 ugani Emirates.

Kabla ya hapo, Arsenal watasafiri hadi Amerika kwa mechi kadhaa za kirafiki zikiwemo dhidi ya Bournemouth, Manchester United na Liverpool halafu warejee jijini London kuvaana na mabingwa wa Ujerumani Bayer Leverkusen pamoja na Lyon kutoka Ufaransa.

Kocha Mikel Arteta atakuwa akichunguza kikosi chake wakati huo wa kujiandaa kwa msimu mpya. Mhispania huyo atatumai kuwa atapata silaha mpya kabla ya msimu kuanza.

Sajili mpya wa Manchester United beki Leny Yoro (kushoto) katika picha hii inayoonyesha uwezekano wa kupangwa na difenda Lisandro Martinez. Picha|Hisani

Arsenal bado hawajasaini mchezaji mpya tangu soko lifunguke Juni 14 hadi Agosti 30.

Zikisalia wiki nne ligi ing’oe nanga, kompyuta maalum imejaribu kubashiri jedwali la mwisho la EPL la msimu 2024-2025.

Kampuni ya kubeti ya Grosvenor Sport imetumia kompyuta hiyo kubashiri jedwali litakavyokaa mwisho wa msimu huo.

Ubashiri huo unaamini kuwa Arsenal bado hawatashinda ligi. Unaamini kuwa vijana wa Arteta watakamata nafasi ya pili kwa alama 86, nane nyuma ya Manchester City wanaopigiwa upatu kunyakua taji kwa mara ya tano mfululizo.

Liverpool wanabashiriwa kumaliza nafasi ya tatu kwa alama 80 nao United wa kocha Erik ten Hag wanapigiwa upatu kufunga mduara wanne-bora.

Kompyuta hiyo maalum inasema kuwa Tottenham Hotspur watamaliza katika nafasi ya saba, Chelsea watakosa Klabu Bingwa Ulaya kwa sababu watakamata nafasi ya tano nao Aston Villa nambari sita.

Kulingana na Grosvenor Sport, Nottingham Forest, Wolves na Ipswich Town ni klabu tatu zitakazoshushwa ngazi.