Dimba

Kenya yajaa wasiwasi kuhusu viwanja maafisa wa CAF wakianza ziara Jumatano

Na JOHN ASHIHUNDU November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUNA wasiwasi kuwa huenda Kenya ikapoteza nafasi ya kuandaa michuano ya CHAN mwaka ujao kutokana na uzembe wa ujenzi kwenye viwanja vilivyopendekezwa kwa mechi hizo za wachezaji wanaosakata soka kwenye ligi za nyumbani.

Kenya pamoja na mataifa jirani — Uganda na Tanzania zimepewa fursa ya kuandaa kwa pamoja michuano hiyo, lakini kuna hofu kwamba ujumbe wa CAF unaozuru nchini kuanzia Jumatano, Novemba 27, 2024 utapata kama haviko tayari.

Mbali na mashindano hayo yaliyotarajiwa kufanyika mwaka huu, vile vile mataifa hayo ya Afrika Mashariki yamepewa idhini kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za 2027.

Kulingana na Kamati ya Kitaifa ya maandalizi ya michuano ya CHAN, ujumbe wa CAF utawasili nchini Jumatano kufanya ukaguzi wake wa pili kwenye viwanja pamoja na vifaa vingine muhimu na kumaliza shughuli hizo mwishoni mwa wiki.

Ujumbe huu unawasili wakati Kenya iko mbioni kutayarisha viwanja vya Nyayo na Kasarani na Talanta Sports Center vilivypendekezwa kwa michuano hiyo kuhakikisha vinafikia viwango vya kimataifa kulingana na matakwa ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

Mbali na viwanja, ujumbe huo utakagua hoteli, viwanja vya ndege, viwanja vya mazoezi miongoni mwa vifaa vingine muhimu. Huu ni ukaguzi wa pili kufanyiwa mataifa hayo wenyeji baada mwingine ulioongozwa na rais wa CAF, Patrice Motsepe kufanyika Septemba, 2024 na kutoa ripoti kwamba uliridhika na maandalizi ya Uganda na Tanzania.

Ujumbe unaozuru nchini unajumuisha maarifa wa CAF kutoka idara ya masoko, mawasiliano, utangazaji, ushindani, usalama wa matibabu itifaki.

Majuzi, ukosefu wa viwanja vya kimataifa nchini ulisababisha kuahirishwa kwa mechi kubwa kati ya AFC Leopards na Gor Mahia maarufu kama Mashemeji Derby iliyoratibiwa kuchezewa Nyayo Stadium, Novemba 24.

Nyayo Stadium ulio na uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 30,000 unafanyiwa marekebisho yanayotarajiwa kumalizika mwezi ujao kwa ajili ya uandalizi wa michuano ya CHAN.

Mbali na Nyayo, MISC Kasarani unaobeba zaidi ya mashabiki 60,000 pia unafanyiwa ukarabati unaotarajiwa kukamilika wiki chache zijazo.

Akizungmza na waandishi wa habari za Michezo, Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana, Kipchumba Murkomen alihakikishia taifa kwamba viwanja hivyo vitakuwa tayari kufikia mwezi ujao.

Alipofanya ziara ya kukagua viwanja hivyo majuzi, Waziri Murkomen alisema viwanja hivyo vitakuwa tayari kufikia mwezi ujao.