Kompyuta ya Opta yasema Arsenal itashinda EPL, Mancheter United nambari 10
MANCHESTER United watakosa tena mashindano yote ya klabu ya Ulaya (Uefa Champions, Europa League na Europa Conference) msimu 2026-2027 ikiwa ubashiri wa kompyuta maalum ya Opta kuhusu maeneo timu 20 zitamaliza kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza 2025-2026.
Baada ya kufanyiwa majaribio 10,000 kuhusu ni wapi timu zitamaliza kwenye ligi hiyo msimu 2025-2026, Opta imesema Oktoba 31, 2025 kuwa wanabunduki wa Arsenal watamaliza ukame wa miaka 20 bila taji kwa kuibuka mabingwa kwa alama 80.
Manchester City ya kocha Pep Guardiola itaridhika na nafasi ya pili kwa alama 69, mbele ya nambari tatu na mabingwa watetezi Liverpool kwa tofauti ya ubora wa magoli. Chelsea watakamata nafasi ya nne na mwisho ya kushiriki Klabu Bingwa Ulaya kwa alama 60. Blues watapiku nambari tano Aston Villa kwa tofauti ya ubora wa magoli. Villa kwa hivyo watashiriki Ligi ya Uropa.
Nafasi ya sita hadi 10 zitashikiliwa na Bournemouth (pointi 59), Newcastle (59), Tottenham Hotspur (58), Crystal Palace (57) na Manchester United ya kocha Ruben Amorim (57). Brighton, Brentford, Everton, Sunderland, Fulham, Leeds na Burnley wataponea msimu mwingine wa Ligi Ku, huku shoka likiangukia Nottingham Forest, West Ham na Wolves.
Ubashiri huo ukitimia utafurahisha mashabiki wa Arsenal ambao mara ya mwisho timu yao ilitwaa taji ni msimu 2003-2004.
Nao mashabiki wa mashetani wekundu wa United watasikitika, hasa kwa sababu msimu 2025-2026 hawashiriki Klabu Bingwa Ulaya, Ligi ya Uropa wala Europa Conference League.
Isitoshe, United pia walibanduliwa kwenye kipute cha Carabao Cup na wanyonge Grimsby Town katika raundi ya pili mwezi Agosti.
Kwa sasa, Arsenal inaongoza ligi kwa alama 22 baada ya michuano tisa ya kwanza.
Bournemouth wanapatikana katika nafasi ya pili kwa alama 18, moja mbele ya Tottenham na Sunderland nao Manchester City na Manchester United wanafuatana katika nafasi ya tano na sita wakiwa na alama 16 kila mmoja.
Liverpool wako nafasi ya saba kwa alama 15, mbele ya Villa kwa tofauti ya ubora wa magoli nao Chelsea na Palace wanafinga 10-bora kwa alama 14 na 13, mtawalia. Forest, West Ham na Wolves wako katika mduara hatari wa timu tatu za mwisho.
