Shabana itakuwa mswaki kwetu, Mihic ajipigia kifua Gor ikitua Gusii
Gor Mahia itavaana na Shabana kwenye mechi kali na kubwa zaidi ya Ligi Kuu (KPL) Jumapili huku mbio za kuwania ubingwa wa msimu huu zikiendelea kupamba moto.
Viongozi Kenya Police (alama 52), Tusker (alama 51) na Gor Mahia (alama 50) zinapambana sana kuwania ubingwa wa KPL huku zikiwa zimesalia mechi sita msimu huu utamatike. Shabana ambayo ina alama 46 pia inapigania ubingwa wa KPL.
Mechi nyingine kali itakuwa kati ya Tusker na AFC Leopards mnamo Jumamosi katika uga wa Kenyatta, Machakos.
Ngarambe kati ya Shabana na Gor itakuwa ugani Gusii na tayari imeibua msisimko mkubwa hasa miongoni mwa mashabiki wa timu zote mbili.
Mashabiki wa Gor mwanzoni hawakutaka mechi hiyo igaragazwe uwanja wa Gusii wakisema ni mdogo huku wale wa Tore Bobe nao wakisema kwamba klabu yao itasusia mchuano huo kama hautapigwa Gusii.
Japo sasa ni dhahiri mechi itachezwa Gusii, itabidii maafisa wa usalama wawe ange kuzuia janga lolote kwa sababu uwanja huo unatarajiwa utafurika na mashabiki pamoja na viongozi wa kisiasa kutoka Nyanza.
Shabana haijawahi kufunga Gor tangu warejee kwenye KPL mnamo 2023. Gor imeshinda mechi mbili huku moja ikiishia sare ya 1-1.
Kuelekea mchuano huo, Kocha wa Gor Sinisa Mihic amelalamikia msongamano wa mechi kwa klabu hiyo ambayo italazimika kucheza mechi tatu ndani ya siku saba kati ya Mei 11-Mei 18.
“Japo tumekuwa na msongamano wa mechi, Shabana hawawezi kutupiga. Lazima tupate ushindi uwanja wa Gusii kivyovyote vile kwa sababu tunapambania taji la KPL,” akasema Mihic, 46 raia wa Croatia.
Gor pia inawania ubingwa wa Mozzart Bet huku Kenya Police wakiwa bado hawajui wapinzani wao kwenye mashindano hayo nao Tusker walibanduliwa kwenye raundi ya 16.
“Baadhi ya mechi zetu zinastahili kusongeshwa mbele kwa sababu kucheza mechi tatu ndani ya siku tatu hakufai wala hatutapumzika. Kuhusu mechi ya Shabana, tumejiandaa vizuri na ninatarajia ushindi kwa sababu lazima tuendelee kupambania taji pia,” akaongeza Mihic.
Kando na mashabiki, Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Raila Odinga wanatarajiwa kuhudhuria mchuano huo.
Ratiba
Jumamosi
Bidco United v Bandari (Kenyatta, Machakos, 1pm)
Tusker v AFC Leopards (Kenyatta, Machakos, 4pm)
Jumapili
Kenya Police v Kariobangi Sharks (Kenyatta, Machakos, 3pm)
Mara Sugar v Ulinzi Stars (Green, Awendo, 2pm)
Kakamega Homeboyz v Posta Rangers (Mumias Sports Complex, Kakamega, 2pm)
Murang’a Seal v Nairobi City Stars (Sportpesa Arena, Murang’a,3pm)
Shabana v Gor Mahia (Gusii, Kisii, 2pm)