Dondoo

Hofu ya ulevi wa jombi yafikisha mke kwa bosi

June 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na LEAH MAKENA

GIAKI, MERU

MAMA wa hapa alishangaza watu wengi alipozuru ofisi alikokuwa akifanya kazi mume wake ili kupata hakikisho kwamba  hakuwa amepigwa kalamu.

Mama alikiri kuwa alishuku  mumewe alikuwa amefutwa kazi kwa sababu mara nyingi alionekana kwa mamapima akibugia mvinyo na kila alipomuuliza alidai  kuwa alikuwa likizoni.

Habari zasema kuwa mama alisikitishwa na tabia ya mumewe ya kurauka alfajiri kana kwamba alikuwa akienda kazini kisha kukita kambi kwa mamapima mchana kutwa.

Hapo ndipo aliamua kufika kwa bosi kubaini iwapo jamaa alifaa kuwa likizoni baada kukosa kutoa cheti cha kuonyesha  alikuwa mapumzikoni.

Siku ya tukio, mama alifika ofisini mapema na kulazimika kusubiri  bosi wa mumewe aliyefika mwendo wa saa nne.

Baada ya kukubaliwa kuongea na bosi, mama alifungua roho na kuelezea hofu yake kuhusu tabia ya polo na  kukiri kuwa ilimpa wasiwasi  ndipo akashuku jamaa alikuwa amepigwa kalamu.

Inasemekana kuwa mama alipata nafuu alipohakikishiwa kuwa jamaa bado alikuwa mfanyikazi wa kampuni hiyo ila bosi akaonya kuwa mwenendo wake ulikuwa unatiliwa shaka na hivyo alitakiwa kurekebisha iwapo hakutaka kumwaga unga.

Hapo ndipo mama alipata nguvu na kuanza mikakati ya kuwafahamisha ndugu za polo wamfanyie kikao ili apunguze ulevi kabla ya kitumbua kuingia mchanga.

Hata hivyo, wosia wa mama ulionekana kama kumpigia mbuzi gitaa kwani polo alikuwa amezama kwenye ulevi na hakuonyesha dalili za kujinasua.

Minong’ono yasema kuwa mama aliapa kufanya vyovyote vile kumtoa kwenye dimbwi la ulevi na akatishia kuondoka iwapo polo asingetambua juhudi zake.

…WAZO BONZO…