Pasta aalika mganga atibu wanawe walevi
Na CORNELIUS MUTISYA
NZAIKONI, MACHAKOS
Pasta mmoja maarufu eneo hili, aliwaacha majirani wakiwa wameduwaa alipomualika mganga nyumbani kwake ili awagange wanawe waliokuwa wamezama katika ulevi wa kupindukia.
Kulingana na mpambe wetu, pasta alikuwa maarufu kwa mahuburi yake yaliyowagusa wengi wakabadili mienendo yao. Hata hivyo, licha ya pasta huyo kusifika mitaani, wanawe wawili walikuwa wakipenda pombe kupindukia.
Walikuwa wakirauka asubuhi na mapema kila siku kwenda kubugia mvinyo na kushinda kwa mama pima mchana kutwa.
Inasemekana kila siku, walikuwa wakirejea nyumbani usiku wa manane wakibwabwaja maneno ya kilevi na kuwatusi majirani.
“Uraibu wa pombe wa wanawe ulimkera mno pasta huyo. Alishindwa hatua ambazo angewachukulia wanawe ili wakomeshe tabia ya ulevi huo wa chakari kwa sababu walikuwa wakimwaibisha,’’ alisema mdaku wetu.
Inasemekana kwamba pasta huyo alijitahidi kiasi cha uwezo wake kuwaombea wanawe wakomeshe ulevi bila mafanikio mpaka akakata tamaa.
Alipowaza na kuwazua, aliona ni heri atundike wokovu kando kwa muda ili atafute suluhisho la kudumu. Alikata kauli kutafuta huduma za mganga amtatulie masaibu yaliyowasibu wanawe.
“Pasta alimualika mganga maarufu kutoka kaunti jirani ili amsaidie kumaliza ulevi wa wanawe. Aliwaacha waumini, majirani na marafiki vinywa wazi kwa sababu kwao alikuwa mfano wa kuigwa,’’ alisema mdaku wetu.
Tunaarifiwa kwamba mganga alitekeleza vimbwanga vyake na kuondoka. Wakazi wanasubiri kuona iwapo vijana hao wataacha pombe.
“Pasta ameacha kuhubiri mitaani kama ilivyokuwa kawaida yake. Wakazi wanashuku huenda akaacha huduma kabisa baada ya kuonyesha imani tofauti na anayohubiri,’’ alisema mdaku wetu.