Habari Mseto

DPP atamatisha kesi ya ulaghai wa Sh520 milioni dhidi ya wakurugenzi


MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga ametamatisha kesi ya ulaghai wa Sh520 milioni dhidi ya wakurugenzi wa hoteli maarufu Nairobi kwa jina Nyama Mama.

Akiwasilisha ombi hilo kwa hakimu mwandamizi Wandia Nyamu, Bw Ingonga alisema kesi hiyo inatokana na mkopo uliopewa kampuni ya-The Good Earth (Group) Limited-TGEG- na Benki ya Victoria (VCB).

Wakurugenzi wa TGEG Bw Jayesh Umedial Shanghavi na mkewe Nina Umedial Shanghavi walidhamini mkopo wa kustawisha biashara yao.

Bw Ingonga alimweleza hakimu kwamba biashara ya Jayesh na Nina ilinonga na walikuwa wanalipa mkopo hadi pale gonjwa la Covid-19 lilipobisha na kuizorotesha jinsi lilivyofanya biashara kote ulimwenguni.

DPP alisema Benki ya VCB ilishtaki TGEG ndipo ilipwe pesa za mikopo miwili iliyoipa 2018 na 2019.

Mahakama ilifahamishwa Jayesh na Nina wameshauriana na VCB na kuelewana jinsi itakavyolipa mkopo huo wa Sh520 milioni.

Wawili hao walikuwa wameudhamini mkopo huo kwa kuipa VCB hati za umiliki wa ardhi na nyumba.

Kwa mujibu wa maelewano kati ya VCB na TGEG, benki hiyo ilikuwa imepewa idhini ya kuwapa ufadhili wakurugenzi hao.

Mawakili Julie Soweto na Jackson Awele hawakupinga ombi la kutamatisha kesi dhidi ya Jayesh na Nina wakisema “wateja wao hawakukataa kulipa mkopo huo ila kesi ya uhalifu waliyoshtakiwa imekuwa kizingiti.”

Bi Soweto na Bw Awele walisema ni heri kesi inayoendelea katika mahakama kuu isuluhishwe kwa vile hatimiliki za wateja wao (Jayesh na Nina) zingali na VCB.

Akitoa uamuzi, Bi Wandia alitamatisha kesi hiyo akisema DPP yuko na mamlaka chini ya kifungu nambari 157 cha Katiba kusitisha kesi wakati wowote kabla ya adhabu kutolewa.

Hakimu alitamatisha kesi dhidi ya Jayesh na Nina kisha aakumuru dhamana waliyolipa ya Sh400,000 warudishiwe.