Habari Mseto

Familia ya Mkenya aliyetekwa nyara DRC yaomba usaidizi aachiliwe

Na FRANCIS MUREITHI September 3rd, 2024 1 min read

FAMILIA ya dereva wa lori Mkenya, Bi Florence Wanza Munyao, 45 kutoka Kaunti ya Machakos, inaomba kumpata mtoto wao akiwa hai baada ya kutekwa nyara na waasi wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la Congo River Alliance (Alliance Fleuve Congo, AFC), Florence alitekwa nyara Agosti 27, 2024 katika eneo la Kiseguro.

“Wanachama wa waasi wa FDLR walimteka nyara dereva wa lori Mkenya Florence Wanza Munyao kutoka Machakos mnamo Agosti 27, 2024, saa sita mchana katika eneo la Kiseguro,” vuguvugu lilisema.

Vuguvugu hilo lililaani FDLR kwa kuzidisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Licha ya hali hiyo ya kusikitisha, AFC ilisisitiza lengo lake la kupambana na ugaidi na kuwalinda wakazi na wageni.

Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama mnamo Jumanne, Septemba 3, 2024 alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa Florence ameachiliwa.

Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, Bw Muthama alitoa wito kwa Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, ambaye pia anahudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni, kuhakikisha kurejea kwa Mkenya huyo akiwa salama.