Habari za Kitaifa

Felix Koskei sasa ndiye kuamua lini jopo la kuteua makamishna wapya IEBC litaanza kazi


MKUU wa Utumishi wa Umma Felix Koskei sasa ndiye ataamua ni lini uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) utaanza.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kuutia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ya 2024 kuwa sheria Jumanne katika ukumbi wa KICC, Nairobi.

Kwa mujibu wa utaratibu katika sheria hiyo, Koskei anatarajiwa kuziandikia asasi zinazotarajiwa kuchangia wawakilishi katika jopo hili ziwasilishe majina yao kwa afisi yake.

Hata hivyo, sheria hiyo haisemi ni muda gani baada kuanza kutumika kwake ambapo Mkuu wa Utumishi wa Umma anapaswa kuziuliza asasi hizo kuwasilisha majina hayo.

Kulingana na sheria hiyo, asasi zinazohitajika kuteua wawakilishi katika jopo hilo ni; Tume ya Huduma za Bunge (PSC), Kamati ya Ushirikishi wa Vyama vya Kisiasa (PPLC), Chama cha Wanasheria Nchini (LSK), Taasisi ya Wahasibu Nchini (ICPAK) na Baraza la Madhehebu Nchini (IRCK).

Tume ya PSC itateua wawakilishi wawili; mmoja akiwakilisha mrengo wa Wengi na mwingine akiwakilisha mrengo wa Wachache.

Ni vyama vyenye angalau wawakilishi 21 katika Bunge la Kitaifa na Seneti ndivyo vinaruhusiwa kuteua wawakilishi katika jopo hilo la kuteua mwenyekiti wa makamishna wa IEBC.

“Ni chama au muungano wenye angalau asilimia tano ya uanachama katika Bunge la Kitaifa na Seneti zinahitimu kuteua wawakilishi katika jopo hili,” sheria hiyo inaeleza.

Kamati ya PPLC itateua wawakilishi watatu; mmoja atatoka chama cha kisiasa au muungano ambao hautambuliwi bungeni, mwingine atatoka chama au muungano unaounda serikali. Mteule wa tatu atatoka chama cha kisiasa au muungano usiounda serikali.

LSK na ICPAK zitateua mwakilishi mmoja, kila moja katika jopo hilo huku baraza la IRCK likiteua watu wawili.

Nafasi ambayo, awali, ilitengewa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) imeondolewa katika sheria hii mpya.

Baada ya afisi ya Bw Koskei kuyapokea majina ya watu hao tisa, watateuliwa rasmi na Rais William Ruto kupitia tangazo kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.

Ni baada ya kuteuliwa kwao ambapo wataapishwa rasmi na Jaji Mkuu Martha Koome na kupewa muda wa miezi miwili kuendesha kibarua cha kuteua mwenyekiti na makamishna sita wapya wa IEBC.

Kulingana na mswada huo, ambao sasa ni sheria, muda wa kuhudumu wa jopo la watu saba lililoteuliwa na Rais Ruto Machi 2, 2023 umefikia kikomo.

Jopo hilo liliongozwa na Kasisi Dkt Nelson Makanda na alisaidiana na wengine ambao ni; Charity Kisotu (Naibu Mwenyekiti) Bethuel Sugut, Novince Euralia Atieno, Evans Misati James, Benson Ngugi Njeri na Fatuma Saman.

Kufikia Aprili 27, 2023 jopo hilo lilipoagizwa kusitisha shughuli zake, kwa muda, kutoa nafasi kwa Kamati ya Kitaifa kuhusu Mazungumzo (NADCO) kuendesha shughuli zake, lilikuwa limepokea maombi kutoka kwa watu kadhaa waliotaka kushindania viti vya mwenyekiti na makamishna wa IEBC.

Kulingana na takwimu za muda zilizotolewa na Dkt Makanda, jopo hilo lilikuwa limepokea majina ya watu 25 waliotaka kujaza nafasi ya mwenyekiti huku wengine 925 wakitaka kushindania nafasi sita za makamishna wa IEBC.

Sheria hii mpya ni moja kati ya tisa zilizopendekezwa na kamati ya Nadco kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti yake.