Habari za Kitaifa

Gachagua: Vita vya kisiasa Mlima Kenya ni pambano kati ya viongozi na wasaliti

Na MWANGI MUIRURI August 26th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametaja mashindano ya kisiasa yanayogubika Mlima Kenya kama yaliyo kati ya viongozi wanaopigania maslahi ya jamii na wasaliti.

Kauli hii huenda ikawakasirisha wakosoaji wake hasa wanaoegemea mrengo wa Rais William Ruto.

Bw Gachagua amewapa makataa ya hadi Disemba 31, viongozi wa kimaeneo ambao “hawasikizi raia” (akirejelea wakosoaji wake) kubadilisha mkondo la sivyo watajipata mashakani katika Uchaguzi Mkuu 2027.

“Mimi ni mtu ninayezunguka vijijini nikisikiza raia. Naweza kuwahakikishia kuwa wapigakura tayari wamefanya maamuzi makuu 2027 na ninahofia baada ya muda wa makataa hayo kukamilika, mtaachwa nyuma,” alisema Naibu Rais katika Kaunti ya Kiambu, Agosti 17.

Huku akiwa na wabunge na magavana wapatao 20 pekee kutoka Mlima Kenya wanaomuunga mkono, Bw Gachagua amekiri kambi yake ni ya walio wachache, kwa sasa, lakini akasisitiza kuwa: “Ni heri niwe na wanajeshi wachache ninaoweza kutegemea kuliko kuwa miongoni mwa vigeugeu.”

Huku akiimarisha kampeni yake inayolenga kuunganisha Mlima Kenya kwa kutuliza hali ya kutoridhishwa eneo hilo, matukio ya hivi majuzi kisiasa ukiwemo ukuruba wa Rais Ruto na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, Naibu Rais anageuza mkondo hatua baada ya nyingine.

Kwa wachanganuzi wengi wa siasa, Bw Gachagua anapolalamika kuhusu mahasimu wake kutoka Eneo la Kati, jina linalowajia mara moja ni Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro – anayeambatana na Rais katika ziara zake nyingi.

Bw Nyoro wikendi alikuwa katika hafla za kumkaribisha mwandani wa Bw Odinga aliyeteuliwa majuzi katika Baraza la Mawaziri, Wycliffe Oparanya.

Katika siku za hivi karibuni, Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri, amegeuka taswira ya kumpinga Naibu Rais Mlima Kenya, huku majibizano kati ya wawili hao yakigeuka upesi mashambulizi ya kibinafsi.

Wawili hao wametumia maneno ya kudhalilishana kiasi kwamba wazee wametangaza mipango ya kuwapatanisha.

“Tungependa viongozi hawa wawili wawe marafiki. Kuna mambo fulani wanayorushiana ambayo yanakiuka kanuni zetu kama jamii. Inaweza kutokea tu ikiwa heshima kati yao imesambaratika. Tutajenga upya heshima hizo,” alisema Mzee wa Baraza la Jamii ya Agikuyu, Wachira Kiago.

Bw Kiunjuri amechukua usukani wa kumshambulia Bw Gachagua alipoachia Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wa akisema Naibu Rais anataka kusakama mustakabali wa eneo hilo kisiasa.

Mtazamo huu umekita katika chama United Democratic Alliance (UDA) ya Rais huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Hassan Omar, akimshutumu Bw Gachagua kwa kujaribu kujipatia cheo cha mlinzi wa eneo hilo.

“Rais na wafuasi wake hatatishwa na mtu aliyejipandisha cheo kama mlinzi. Hakuna mtu atakayeshikilia funguo za eneo lolote ifikapo 2027 kwa sababu Wakenya wamekata kauli kuwa wanataka mitazamo ya kitaifa kufanikisha serikali za siku za usoni,” alisema Bw Omar, akitetea mkutano wa Rais Ruto uliofanyika ikulu na viongozi kutoka Mlima Kenya ambapo Naibu Rais hakuwepo.