Habari za Kitaifa

Gen Z walivyolazimisha Raila kukunja mkia kuhusu mazungumzo

Na JUSTUS OCHIENG July 16th, 2024 2 min read

KIONGOZI wa Azimio la Umoja Raila Odinga anakabiliwa na kitendawili kigumu huku akitathmini mahusiano yake na serikali ya Rais William Ruto.

Bw Odinga amejipata kwenye kikaangio moto baada ya kuunga mkono mazungumzo baina ya sekta mbalimbali yaliyoitishwa wiki iliyopita na Rais Ruto kama njia ya kutuliza joto la kisiasa kufuatia maandamano ya Gen Z, ambao wameitisha mabadiliko makubwa katika utawala wa Kenya Kwanza.

Japo mwanzoni Bw Odinga alipigia debe mazungumzo hayo katika hotuba ya pamoja aliyotoa Rais na vinara wengine wa upinzani, kiongozi huyo wa ODM anakabiliwa na shinikizo kuu za ndani kwa ndani kutoka kwa muungano wake wa Azimio.

“Tumeafikiana kuwapa watu fursa ya kusikika na kuelezea malalamishi yanayoathiri taifa letu ili suluhisho la kudumu lipatikane,” alisema wiki jana katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Jijini Nairobi, KICC.

Ajabu ni kuwa, Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka aliyekuwepo KICC, hakushiriki hotuba ya pili ambapo Bw Odinga alikubali mazungumzo, huku akiungana na vinara wengine wa upinzani kumshinikiza kiongozi wa ODM dhidi ya mazungumzo hayo.

Jumapili, Julai 14, 2024 Bw Odinga alizuru eneo la Kware katika vitongoji duni vya Mukuru Kwa Njenga, Nairobi, ambapo miili ya watu wasiojulikana ilipatikana ikiwa imekatwakatwa na kuwekwa kwenye magunia.

Vijana waliokuwa wanaimba nyimbo za kukashifu serikali walimlazimu Odinga kujitenga na mazungumzo yanayoendeshwa na serikali yaliyotarajiwa kuanza jana, Jumatatu, Julai 15, 2024.

“Wale wamewatendea watu wetu ukatili huu ni wanyama. Kama Azimio, hatuwezi kushiriki mazungumzo na watu ambao mikono yao imelowa damu ya vijana wasio na hatia,” Bw Odinga alisema huku vijana wakiimba “hakuna mazungumzo”.

Alisisitiza, “Mikoni yao imelowa damu. Hatuwezi kuzungumza na watu kama hao. Ndiyo sababu ninasema “hakuna mazungumzo!”

Kumekuwepo ripoti kwamba Rais Ruto anatafakari kuhusu “Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” na huenda akajumuisha viongozi wa upinzani katika serikali ya Kenya Kwanza kama njia ya kutuliza joto la kisiasa.

Japo baadhi ya vyama tanzu vya Azimio vimekataa uwezekano wowote wa kujumuika na serikali kwa mazungumzo, ODM ya Odinga ilikuwa imeunga mkono mazungumzo hayo ikisema yatawapa Wakenya fursa ya kusaka suluhu kwa baadhi ya masuala yaliyotajwa katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 yaliyofanyika majuzi.

ODM inaonekana kupania kushiriki mazungumzo hayo baada ya Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) kuidhinisha hatua hiyo Ijumaa iliyopita.

Hii leo, ODM ina kikao cha pamoja na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) na Kundi la Bunge ambapo inatarajiwa pakubwa kupitisha uamuzi wa CMC.

Mkutano wa vinara wa muungano wa Azimio uliotarajiwa kufanyika jana baada ya kikao kilichoandaliwa Jumamosi usiku mjini Kakamega ili kuafikiana kuhusu mazungumzo hayo, haukufanyika.

Taifa Dijitali imebaini kuwa viongozi wa ODM walionya kuhusu mkutano huo wakihoji kuwa kama chama “kujitenga na mazungumzo ni sawa na kutelekeza wajibu wakati ambapo nchi inaitisha mazungumzo.”