• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
2019: Sarakasi bungeni hazikukosa hata Akothee na minisketi yake

2019: Sarakasi bungeni hazikukosa hata Akothee na minisketi yake

Na CHARLES WASONGA

VIOJA na sakarasi hazikukosekana katika majengo ya bunge na kuwaacha wengi vinywa wazi kwa mshangao mkuu.

Mnamo Juni 13, ripoti ziliibuka kwamba Mwakilishi Mwanamke wa Wajir Fatuma Gedi alishambuliwa na mwenzake wa Wajir Mashariki Rashid Amin kwenye sehemu ya maegesho ya magari katika majengo ya bunge.

Katika kisa hicho, ambacho kiliripotiwa kwa polisi na kesi kufunguliwa, ilidaiwa Bw Amin alimzaba kofi Bi Gedi huku akimfokea kwa maneno makali kwa lugha ya Kisomali.

Ilidaiwa kuwa Bw Amin ambaye alichaguliwa bungeni kwa tiketi ya chama cha Wiper alimkabili Bi Gedi, ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, akitaka kujua ni kwa nini eneo-bunge lake (Wajir Mashariki) halikutengewa fedha za ujenzi wa barabara katika bajeti ya kitaifa.

Mbunge wa Wajir Mashariki Rashid Amin alitiwa nguvuni Alhamisi usiku kwa madai ya kumshambulia mwakilishi huyo wa kaunti katika majengo ya Bunge.

Baadaye siku hiyo jioni, Bw Amin alikamatwa na kuhojiwa katika kituo cha polisi cha majengo ya bunge. Naye Bi Gedi alikimbizwa hadi katika Hospitali ya Karen kutafuta huduma za matibabu.

Siku hiyo suala hilo lilijadiliwa bungeni ambapo wabunge wote wanawake waliungana kumkashifu Bw Amin sio tu kwa kushusha hadhi ya bunge bali kumdhulumu Bi Gedi kwa “sababu ni mwanamke”

Naye Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alishutumu kisa hicho na kuwaonya wabunge, hasa wanawake, dhidi ya kugeuza majengo ya bunge “kuwa uwanja wa vita.

Na mnamo Agosti mwaka huu, shughuli za bunge la kitaifa zilitatizwa kwa muda baada ya Mwakilishi Mwanamke wa Kwale Zulekha Juma Hassan kuingia bungeni akiwa na mtoto wake mchanga.

Hatua hii ilimlazimu spika wa muda Chris Omulele kumwagiza kuondoka ukumbini kwa kukiuka kanuni za bunge, agizo ambalo lilipingwa na wabunge wanawake pamoja na baadhi ya wenzao wanaume.

Akitoa agizo hilo, Omulele alitaja kitendo hicho kuwa cha kwanza kuwahi kushuhudiwa bungeni na ni dharau kwa bunge.

Kiongozi wa wengi, Aden Duale alimtaka spika huyo wa muda kuwaagiza maafisa wa ulinzi kwenye bunge hilo kueleza ni kwa nini walimruhusu mbunge huyo kuingia na mwanawe mchanga hadi ndani ya ukumbi wa mijadala.

Kauli yake iliungwa mkono na Kiongozi wa Wachache John Mbadi, ambaye alisikitishwa na ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wabunge.

Akijitetea kuhusiana na kitendo hicho, Bi Hassan alisema kuwa aliamua kuja na mwanawe kazini kwa sababu mjakazi wake hakuwepo siku hiyo na “sikutaka kukosa kufika kazini”.

Baadaye Oktoba 28, mwanamuziki mashuhuri Esther Akoth, maarufu kama Akothee, alisababisha kioja katika majengo ya bunge alipoingia humo akiwa amevalia sketi fupi.

Hii ni kinyume na sheria kuhusu mavazi katika asasi ambayo hutumiwa kutunga sheria za nchi. Sketi hiyo ya rangi ya kijani kibichi, ilikuwa haijafunika magoti kama inavyohitajika kulingani na kanuni hizo. Hali hiyo iliwatia kiwewe walinzi wa bunge wasijue namna ya kumdhibiti msanii huyo ikizingatiwa kuwa wenzao wanaolinda lango kuu tayari walikwisha kumruhusu aingie.

Bi Akothee ambaye alikuwa amealikwa na Mbunge Maalum David Sankok alisema alifika bungeni “kuwasihi wabunge waunge mkono shughuli za wakfu wake za kuchanga fedha za kuwasaidia wahanga wa njaa katika Kaunti ya Turkana.

Walinzi wa kike, walijaribu kumshawishi Bi Akothee akubali kufunika mapaja yake kwa leso “ili aonekane nadhifu lakini akakataa.

Mwanamuziki huyo alijaribu kujitetea akisema kuwa mavazi yake hayakuwa na dosari yoyote huku akiungwa mkono na mwenyeji wake, Bw Sankok.

Hatimaye alisalimu amri, na kufunga leso, baada ya kubembelezwa na wabunge Rachael Nyamai (Kitui Kusini) na Soipan Tuya (Mbunge Mwakilishi Mwanamke wa Narok) waliomwelezea umuhimu wa wageni kuzingatia kanunu kuhusu mavazi bungeni.

You can share this post!

2019 ulikuwa mwaka wa mauaji ya kifamilia

2019: Kamatakamata ya kila Ijumaa ilitesa mafisadi

adminleo