Hatutahudhuria mkutano wa BBI Mlima Kenya – Kuria
Na NDUNG’U GACHANE
MBUNGE wa Gatundu Kusini, Moses Kuria amesema idadi kubwa ya wabunge wa Mlima Kenya hawatahudhuria mkutano wa viongozi wa eneo hilo ulioitishwa na Wakfu wa Mlima Kenya kufafanua ripoti ya jopo la maridhiano (BBI).
Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Kuria alisema licha ya wao kupata mwaliko wa kuhudhuria mkutano kesho katika mkahawa wa Ole Sereni, hawatafika kutokana na kile alichodai ni kutengwa kwao katika mikutano ya awali.
“Hawakutuhusisha katika maandalizi ya mkutano wa Sagana na waliwaweka mbele wabunge wa ODM wakati wa mkutano wa kuzindua ripoti ya BBI katika ukumbi wa Boma. Wawaalike John Mbadi, Gladys Wanga na Sabina Chege,” akasema.
Bw Kuria alisema wabunge kutoka Mlima Kenya walifanya mkutano wao mjini Embu mwisho wa wiki jana na hivyo hawana haja ya kufanya mkutano mwingine wa kuhusu BBI.
Mkutano huo wa Embu ulihudhuriwa na zaidi ya wabunge 40 pamoja na maseneta kadhaa.“Tulifanya mkutano wetu Embu na tunaendelea kutekeleza maamuzi yetu,” akasema.Waandalizi wa mkutano wa Ole Sereni waliwatumia wabunge wote wa Mlima Kenya ujumbe wa kuwaalika.
Kulingana na ujumbe wa kuwaalika viongozi kwenye mkutano huo, waandalizi wengine wa mkutano ni Naibu Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Cecily Mbarire, mwenzake wa Seneti Irungu Kang’ata na Naibu Msimamizi wa Wafanyakazi katika Ikulu, Njee Muturi.
Wanasiasa wa eneo hilo la Kati wamegawanyika tangu handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.