Habari Mseto

Mswada wa kuboresha kilimo cha majanichai washabikiwa na wengi

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

MSWADA wa kuboresha zao la majani chai ulipongezwa na wengi huku mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle” Wainaina akisema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwa sababu wakulima watapata afueni kwa kufaidika na jasho lao.

“Kwa muda mrefu tumeona ya kwamba wakulima wa majani chai wakipunjwa kwa kulipwa pesa kidogo bila kunufaika pakubwa na zao hilo,” alisema Bw Wainaina.

Alisema hatua hiyo imeondoa mawakala na walaghai ambao lengo lao kubwa lilikuwa ni kuwapunja wakulima hao huku wao wakinufaika wenyewe.

“Tunajua wakulima wakipewa nafasi nzuri ya kuendesha kilimo cha zao hilo bila shaka watapata pesa za kuweka mfukoni na kusaidia pia familia zao,” alisema mbunge huyo mnamo Ijumaa mjini Thika.

Mwezi mmoja uliopita Waziri wa kilimo Bw Peter Munya, alizuru eneo la Gatundu Kaskazini ili kujua matatizo halisi yanayopata katika zao la chai.

Katika hafla hiyo wakulima wapatao 1,000 walikongamana katika uwanja wa shule ya Ndiko eneo la Gatundu, ambapo walitoa malalamishi yao kwa uwazi.

Bw Munya kwa kauli moja aliwahakikishia wakulima hao kuwa yeye atahakikisha kuwa hali ya hapo awali ya wakulima wa majanichai kupata haki yao itarejelewa mara moja.

“Mimi najua kwa muda mrefu walaghai wengi hushirikiana pamoja kuona ya kwamba mkulima wa majanichai anazidi kuumia huku wao wakijinufaisha na jasho lao,” alinukuliwa akisema Bw Munya.

Wakati wa mkutano huo waziri huyo alipendekeza ya kwamba sheria mpya iliyotarajiwa kupitishwa bungeni ni kwamba mkulima yeyote akipeleka chai yake kiwandani anastahili kulipwa chini ya wiki moja.

Wakulima wengi walikiri ya kwamba wamepunjwa kwa muda mrefu ambapo zao hilo halijawanufaisha. Walisema mawakala wengi wanaendesha magari makubwa huku wao wakibaki pweke bila chochote.