Afrika yashauriwa kukoma kuwanyima vijana nafasi maishani
NA ALLAN OLINGO
VIONGOZI wa bara Afrika wamehimizwa kupatia kipaumbele masuala yanayohusu vijana.
Suala hilo lilijitokeza katika kongamano linaoendelea nchini Rwanda la Kusi Ideas Festival, kuhusiana na masuala ya Bara Afrika katika kipindi cha miaka 60 ijayo.
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Dkt Mukhisa Kituyi aliwasisimua waliohudhuria kongamano, akisema kizazi cha sasa kinatilia maanani ushirikiano badala ya mashindano ili kufanikiwa.
Dkt Kituyi alisema bara hili linafaa kuwaruhusu vijana kutangamana, kuwekeza na kuhamia taifa moja hadi jingine bila kuwekewa vikwazo vya usafiri na kutangamana.
“Hawa vijana wanatafuta nafasi ya kupata riziki si katika mataifa yao ya kuzaliwa pekee bali hata nchi za mbali. Wanaangalia mbali wanapojizatiti kutimiza ndoto zao na hulazimika kuelekeza macho yao kwenye nafasi za kujiinua zinazopatikana kwingine. Serikali za mataifa ya Afrika zinafaa kutambua hilo kisha kuondoa vikwazo vya usafiri au kutangamana,” akasema Dkt Kituyi.
Marais wa nchi mbalimbali barani pia waliombwa kushirikiana na kufungua mipaka ya mataifa yao kwa raia kutoka nje ili kuwaruhusu kufanya biashara na kuinua uchumi wa nchi husika.
“Tunafaa kuelewa kwamba asilimia 53 ya raia wanaohamia mataifa yetu mbalimbali hapa barani ni Waafrika wenzetu. Wahamiaji hawa ni wa manufaa kwa nchi zao asili na zile wanazohamia kutokana na uwezo wao wa kuwekeza. Haya ndiyo masuala yanayofaa kupigiwa debe badala ya mashindano yasiyozalisha chochote,” akaongeza Dkt Kituyi.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Maendeleo Nchini Rwanda(RDB), Bi Clare Akamanzi alisema mataifa hayafai kuhofia kuondoa vikwazo vya mipaka, akisema uhuru wa kufanya biashara utasaidia kustawisha nchi za Afrika.
“Hakuna sababu maalum ya kuogopa kufungua mipaka yetu. Kama Rwanda tumekuwa tukipigia upato suala hili kwa muda wa miaka mitano iliyopita na limetufaa sana kwa kuwa tumewavutia wageni na wawekezaji wengi,” akasema Bi Akamanzi.
Mwanachama wa bodi ya kampuni ya Msingi East Africa, Bw Linus Gitahi naye alitaka serikali za Afrika kuelekeza macho katika uundaji wa mtaala mpya unaosisitiza matumizi ya teknolojia kuendesha masuala ya nchi.