Afueni baada ya masoko Githurai kufunguliwa
NA SAMMY WAWERU
Wafanyabiashara wa masoko ya Githurai wamepata afueni baada ya kuruhusiwa kuendeleza shughuli zao, wiki mbili baada ya masoko yote eneobunge la Ruiru kutakiwa kufungwa.
Kwenye barua, soko la Jubilee na Migingo, soko la Ruiru mjini, pamoja na wachuuzi wenye vibanda barabarani walitakiwa kusitisha shughuli zao kwa muda wa siku 21, kuanzia Machi 26, 2020, ili kusaidia kudhibiti maambukizi ya Covid – 19.
Walioathirika na amri hiyo ni wauzaji wa nguo, wanaouza bidhaa za kula wakitakiwa kuendeleza shughuli zao ila kwa kuzingatia utaaratibu na maagizo yaliyotolewa na serikali. Kadhalika, wenye maduka ya huduma za kutoa na kuweka pesa ndiyo M-Pesa walisazwa.
Kwenye uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali mnamo Jumatano, imebainika wafanyabiashara wa nguo wa masoko yaliyotajwa wameruhusiwa kundeleza gange zao japo kwa kuzingatia maagizo. “Ilani iliyotolewa imefutwa kwa muda. Tumeruhusiwa kuendesha kazi kwa masharti ya kuzingatia usafi na umbali baina ya mtu na mwenzake,” akasema Jecinta Wangui, muuzaji wa viatu katika soko la Jubilee.
Serikali inaendelea kuhimiza umma kutilia maanani utaratibu uliotolewa na wizara ya afya, hasa kuzingatia kigezo cha umbali wa zaidi ya mita moja, kunawa mikono ikiwa ni pamoja na kuvalia vitamvua kufunika pua na mdomo.
Ikizingatiwa kuwa uchumi na biashara zimeathirika kwa kiasi kikuu tangu kisa cha kwanza cha Covid – 19 kuripotiwa hapa nchini, Mercy Nyambura ambaye pia huuza viatu alisema wanalemewa kununua jeli ya kunawisha wateja. “Mauzo tunayopata ni ya kutukidhi mahitaji ya kimsingi, hasa chakula, hayatoshi kununua jeli za kunawisha wateja,” Nyambura akalalamika. Wengi wao wamejihami na jeli zao binafsi, ili kunawa mikono wanapopokea pesa.
Kulingana na Bw Martin Kamau, anayeuza mavazi, alisema kiwango cha mauzo kimeshuka baadhi ya siku wakikosa kupata wateja.
Kwenye uchunguzi, ni wachache mno wenye mitungi ya maji yaliyotibiwa na sabuni watu kunawa mikono. “Kabla kuhudumia mteja sharti anawe mikono,” akasema Antony Kabue, mhudumu wa M-Pesa.
Wauzaji wa bidhaa za kula wanaendeleza biashara kama kawaida, japo wanasema muda wa kafyu unafungia nje wateja wengi. Kafyu ya kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhu inaendelea kutekelezwa kote nchini.
Licha ya wauzaji nguo za mitumba kuruhusiwa kufungua biashara, vibanda kadhaa vimesalia kufungwa kwa kukosa kufanya mauzo wanapofungua. Mercy Nyambura alisema kuuza pea mbili ya viatu kwa siku ni kwa neema ya Mungu. “Kuna siku ninakosa kufungua kwa hofu ya kushinda mchana kutwa bila kuuza chochote,” akasema mfanyabaishara huyo, akiongeza kwamba mambo yakiendelea yanavyoonekana huenda wengi wakashindwa kukidhi familia zao na kulipa kodi ya nyumba.
Wafanyabiashara wa nguo tuliozungumza nao walisema hali inayoshuhudiwa eneo hilo ni sawa na ya soko maarufu la Gikomba, Nairobi ambako hununua nguo kwa bei ya kijumla, wakilalamikia zinakosekana.
Kufikia sasa Kenya imethibitisha kuwa na zaidi ya wagonjwa 170 wa virusi hatari vya corona, sita wakiripotiwa kuaga dunia. Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mnamo Jumanne alionya taifa lijiandae kwa visa zaidi ikiwa watu hawatatii maagizo na utaratibu uliotolewa.
Kudhibiti maambukizi zaidi, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza safari za kuingia na kutoka kaunti ya Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale, kusitishwa kwa muda wa siku 21. Katika kaunti ya Nairobi, amri hiyo ilianza kutekelezwa mnamo Jumatatu, Mombasa, Kilifi na Kwale ikitarajia kuanza kutekelezwa Jumatano. Aidha, agizo hilo pia linahusisha sehemu kadhaa kaunti ya Kiambu.
Magari ya kusafirisha bidhaa za kula na dawa, ndiyo pekee yanaruhusiwa kuingia kaunti zilizotajwa.