Habari Mseto

Ahadi nyingine ya Ruto kuajiri vijana 50,000 kusafisha mito Nairobi

Na SAMMY WAWERU March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ametoa ahadi ya kuajiri vijana 50,000 kusaidia katika oparesheni kusafisha mito Nairobi.

Kiongozi wa nchi alitoa ahadi hiyo Alhamisi, Machi 14, 2025 kwenye ziara yake mtaani Kibra, Nairobi.

Rais Ruto wiki hii amefanya ziara katika mitaa mbalimbali Nairobi, ambapo amezindua miradi kadha ya maendeleo huku akitoa ahadi tele kwa wananchi.

Akihutubia umma katika mtaa wa mabanda wa Kibra, aliahidi kuwa serikali yake itaajiri vijana wapatao 50,000 kusaidia kung’arisha mito Nairobi.

“Kupitia mpango wa kusafisha mito Nairobi, tunataka kuajiri vijana 50,000,” Dkt Ruto alisema.

Kwenye idadi hiyo, aliahidi wakazi wa Kibra kwamba itajumuisha vijana na kina mama kutoka mtaa huo.

“Vijana wa Kibra na kina mama pia watanufaika,” Rais alielezea.

Ahadi ya Ruto kwa vijana Kibra inajiri siku chache baada ya kutoa nyingine kwa wanafunzi Nairobi.

Rais alimtaka Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja kutafuta mashine ya kupika chapati 1,000,000, ili kupiga jeki programu yake ya ‘Dishi na County’.

Bw Sakaja alidai changamoto inayozingira mpango huo ni ukosefu wa mashine inayoweza kupika chapati kulisha wanafunzi 300,000.

Ni programu ambayo Gavana Sakaja amekuwa akiendeleza katika shule za upili za umma Nairobi, kulisha watoto.

Ahadi ya Ruto kununua mashine itakayounda chapati 1,000,000 imepokea hisia mseto mitandaoni, Wakenya wakichora vibonzo vya kumkejeli kiongozi wa nchi.

Dkt Ruto amekuwa akikosolewa na Wakenya kwa kutoa ahadi nyingi ambazo hatimizi, tangu wakati wa kampeni 2022 na alipotwaa mamlaka.