Habari Mseto

Ajabu kituo cha polisi kikifungwa kwa kushindwa kulipa kodi

Na GEORGE MUNENE March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KITUO cha polisi cha Riandira Kaunti ya Kirinyaga kimefungwa kwa muda usiojulikana kutokana na malimbikizi ya kodi Sh2 milioni.

Kituo hicho kimekuwa kikiwahudumia wakazi kwa takriban miaka tisa katika jengo la kibinafsi.

Kufungwa kwa kituo hicho muhimu mnamo Machi 24, kuliwafanya wakazi wa soko la Riandira na viunga vyake kuwa na hofu.

Polisi walionekana wakibeba virago vyao na kuondoka, jambo lililowashangaza wakazi hao.

“Maafisa hao wameondoka na hatujui walikokwenda, kwa kweli waliimarisha usalama katika eneo hili na tutateseka,” mmoja wa wakazi Bi Grace Wanjiru alisema.

Mnamo 2016, tajiri wa eneo hilo, marehemu Mwangi Thuita alitenga jengo hilo kwa polisi kuanzisha kituo cha polisi kufuatia kuongezeka kwa visa vya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Polisi walipaswa kuendelea kulipa kodi na kuondoka katika jengo hilo baada ya serikali kujenga kituo chake cha polisi katika eneo hilo.

Hata hivyo, serikali haijaweza kujenga kituo chake cha polisi na maafisa wake wa usalama waliendelea kufanya kazi kwenye jengo la kibinafsi bila kulipa chochote hadi tajiri huyo alipokufa mnamo 2018.

Lakini familia ya tajiri huyo ilichoka na kuwafurusha maafisa wa polisi, na kusababisha kufungwa kwa kituo hicho.

“Kabla ya baba yetu kufariki, alituambia kuwa maafisa waliokuwa katika kituo cha polisi walipe kodi. Maafisa hao waliendelea kumiliki jumba hilo bila kulipa kodi na ikabidi waondoke ili tukodishe jengo hilo kwa mtu mwingine,” alisema Bi Irene Njeri, bintiye marehemu.

Wakazi wanahofia kuwa ukosefu wa usalama utarejea katika eneo hilo kwani maafisa wa usalama wamehamishwa kufuatia kufungwa kwa kituo hicho.

“Kituo hicho kimekuwa muhimu kwetu, sasa tumeingiwa na hofu kwa sababu hakuna maafisa wa usalama wa kukabiliana na wahalifu, tangu kifunguliwe, tumekuwa tukiishi kwa amani na visa vya uhalifu vilipungua lakini sasa huenda majambazi wakaanza kuvamia nyumba zetu na maeneo ya biashara,” akaongeza Bi Wanjiru.

Wakazi wa eneo hilo sasa wanaomba serikali kuingilia kati na kujenga kituo cha polisi kitakachoimarisha usalama.

“Serikali inafaa kuharakisha na kuweka kituo kipya cha polisi katika eneo hilo kabla ya majambazi kuanza kututia hofu na kutuhangaisha,” alisema Bw Francis Gikongo.