• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
Ajisaliti kuweka benki mamilioni ya pesa za wizi kila siku

Ajisaliti kuweka benki mamilioni ya pesa za wizi kila siku

NA SAM KIPLAGAT

AFISA wa zamani wa Kaunti ya Nairobi aliyejisaliti kwa kuweka benki mamilioni ya pesa kila siku, ameagizwa na mahakama arejeshe mamilioni aliyoiba.

Jimmy Kiamba, ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Fedha katika kaunti hiyo, hakuweza kufafanulia mahakama jinsi alivyopata mamilioni aliyoweka kila siku, ikizingatiwa kuwa mshahara wake ulikuwa Sh85,000 kwa mwezi.

Jaji Hedwig Ong’udi vile vile alimwagiza Bw Kiamba alipe Sh35 milioni kwa serikali la sivyo nyumba yake ya kifahari katika mtaa wa Runda ichukuliwe.

“Naagiza serikali ilipwe Sh282,648,604 na mshtakiwa,” akaamuru Jaji Ong’udi.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ambayo iliwasilisha kesi hiyo, iligundua kwamba Bw Kiamba hakuweza kufafanua zilikotoka Sh317,648,604 pesa taslimu zilizowekwa kwenye akaunti yake nyakati tofauti na maafisa wa kaunti.

Afisa huy,o ambaye alihudumu chini ya aliyekuwa gavana Dkt Evans Kidero, awali alikuwa amewaeleza maafisa wa EACC kwamba alipata fedha hizo kutokana na mauzo ya ng’ombe, mawe ya ujenzi na ngano na biashara za uchukuzi.

Hata hivyo, Jaji Ong’udi alisema ilikuwa vigumu kujua kiasi cha fedha ambazo ziliwekezwa na afisa huyo kwenye biashara ya uchukuzi, ndiyo maana nyumba aliyonunua kwa Sh35 milioni iliwekwa chini ya mali ambayo maelezo ya jinsi ilivyopatikana yalikosa kuridhisha.

Mahakama ilielezwa kwamba EACC ilichunguza akaunti 11 za Bw Kiamba, ambazo zipo kwenye benki nane, na pia kuchunguza nakala ya jinsi alivyoweka na kutoa pesa. Ilipolinganishwa na mshahara wake, ndipo ikafikia uamuzi kwamba mali yake haikupatikana kwa njia halali.

Kati ya Januari na Novemba mwaka wa 2014, EACC ilipata kwamba Bw Kiamba alikuwa na Sh400 milioni kwenye benki, ilhali alikuwa akilipwa mshahara wa Sh85,000 kila mwezi akihudumu kwenye wadhifa wake.

Miaka michache baadaye, ilishangaza kwamba mshahara wake uliongezeka hadi Sh1.09 milioni kila mwezi na nyumba za kukodisha alizojenga mtaa wa Athi River pia zikimletea Sh2.7 milioni kwa mwezi.

Kati ya wafanyakazi wa kaunti ambao EACC ilipata na hatia ya kuwatumia kuweka pesa kwenye akaunti zake nyakati tofauti ni Joseph Njoroge (Sh66.8 milioni), Stephen Osiro (Sh4.1 milioni), Barnabas Ougo (Sh15.65 milioni), Ambrose Musau (Sh3.4 milioni) na Joseph Njoroge (Sh1.3 milioni).

Hata hivyo, korti ilieleza kushawishika na jinsi Bw Kiamba alivyopata mali yake nyingine kama nyumba maeneo ya Naivasha na Muthaiga.

You can share this post!

Kashfa zatia doa uteuzi wa mawaziri

Kenya kuuza mafuta ng’ambo chini ya mpango wa majaribio

adminleo