Habari Mseto

Mkenya na Watanzania wakana kuiba mamilioni

April 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Levanda Akinyi almaarufu Ruth Wairimu (kushoto) akiwa kizimbani na raia wa Tanzania Teresa Richard, Rose Richard na Shimton Ambasa Aprili 11, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE anayeshukiwa kushirikiana na majambazi kutoka nchini Tanzania alishtakiwa Jumatano kuwanyang’anya wawekezaji kutoka Uchina pesa na mali ambayo thamani yake ni zaidi ya Sh18.4 milioni mwezi Machi, uvunjaji wa nyumba na wizi wa mali na pesa zenye thamani ya Sh8 milioni.

Bi Levanda Akinyi Ogilo alifikishwa kortini baada ya hakimu mkuu wa Nairobi Bw Francis Andayi kuwaamuru polisi wamfungulie mashtaka baada ya kumzuia rumande kwa muda wa wiki moja.

Bi Akinyi alishtakiwa pamoja na raia watatu wa Tanzania Bi Teresa Richard , Bi Rose Richard, na Shimton Ambasa Khan.

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka zaidi ya kumi ya kuvunja nyumba na kuiba mali na pesa kutoka kwa Mabw Zhang Gong , Wan Baihui, Bi Zhia Qian, Moses Kironyo Pratt na  Mohamud Hussein Egeh.

Washtakiwa hao wanne walikana kuiba vipakatalishi, Dola za Kimarekani, Euro na sarafu za Uchina zote zenye thamani ya zaidi ya Sh18,463,000.

Wakili John Swaka anayewakilishtakiwa hao wote aliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana akisema Akinyi ni mama aliyeacha watoto kwa nyumba.

Bw Swaka alisema washtakiwa hao walitiwa nguvuni Machi 30,2018 na wamekuwa wakizuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

Jambo hilo lilimuudhi Bw Andayi ndipo akamwagiza kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha apeleke uamuzi wa mahakama kuu katika kila kituo cha polisi jijini Nairobi unaosema hakuna mshukiwa wa wizi au kosa lingine lolote anayepasa kuzuiliwa kama hakuna shtaka la kumshikilia.