Habari Mseto

Aliyejifanya Sabina Chege kuwatapeli wabunge kupimwa akili

April 3rd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyekamatwa wikendi kwa madai ya kutumia jina la Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege kuwatapeli wabunge wengine pesa alifikishwa kortini Jumanne.

Hata hivyo mshukiwa Wazir Benson Masubo almaarufu Wazir Chacha, ambaye alitiwa nguvuni nchini Tanzania, hakusomewa mashtaka alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi katika mahakama ya Milimani, Nairobi Bi Christine Njagi, kwa vile polisi waliomba muda wa siku saba kumhoji.

Inspekta John Kiprop kutoka kituo cha Polisi cha Bunge alimtia nguvuni Bw Masubo eneo la Tarime nchini Tanzania.

Wiki iliyopita, mahakama ilikuwa imetoa kibali cha kumtia nguvuni Masubo kwa makosa ya kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu.

Hakimu Njagi alifahamishwa kuwa mshukiwa huyo alitiwa nguvuni Machi 30, 2018 na polisi hawakuwa na muda wa kutosha kumhoji na kuandika taarifa kutoka kwa mashahidi ambao wengi ni wabunge wanawake.

“Naomba mahakama iamue mshukiwa azuiliwe katika kituo cha polisi ili tumhoji na pia taarifa ziandikishwe kutoka kwa Bi Chege na walalamishi wengine aliojaribu kupokea pesa kutoka kwao akitumia jina la mbunge huyo,” akaomba Bw Kiprop.

Lakini wakili Job Ngeresa anayemtetea Bw Masubo alipinga ombi la mteja wake kuzuiliwa kwa muda wa siku saba.

“Mshukiwa alikamatwa Machi 30, 2018 na amekuwa mikononi mwa polisi,” akasema na kuomba mshukiwa aachiliwe kwa dhamana ili aweze kuenda hospitali kutibiwa, kwa vile anaugua maradhi ya ubongo yajulikanayo kwa lugha ya Kiingereza – Migrane.

“Mshukiwa huyu hakuwa akitoroka mbali alikuwa anaenda hospitali ya Muhimbili iliyoko mjini Dar-es-Salaam kupokea matibabu ya kichwa.

Mara kwa mara amekuwa akienda nchini Tanzania kusaka tiba ya kichwa kwa vile anapoanza kuugua yeye hutoa nguo akaachwa uchi wa mnyama,” Bw Ngeresa alimweleza hakimu.

Wakili huyo aliomba korti iamuru apelekwe hospitali ya Mathare kupimwa ikiwa ni mwendawazimu na ripoti iwasilishwe Aprili 9, 2018 atakaposhtakiwa.