• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Asimulia sasabu ya kugura kazi ya upishi akawa mwosha kwa mochari

Asimulia sasabu ya kugura kazi ya upishi akawa mwosha kwa mochari

Na PHYLLIS MUSASIA

Uraibu wake wa kupika vyakula mbalimbali vilivyoongezwa ladha na kurembeka, ndio kazi iliomwezesha kupata riziki ya kila siku.

Sarah Nyambura mwenye umri wa miaka 35, alilazimika kujifunza maswala ya upishi akiwa na umri mdogo baada ya wazazi wake kuaga dunia na kuwaacha ndugu zake chini ya ulinzi wake.

“Mimi ndiye mkubwa kwa ndugu zangu wote. Wazazi walipoaga dunia katika ajaliya barabara, ilinibidi nishike ushakani wa kuwachunga wenzangu licha ya umri wangu mdogo. Hapo ndipo nilianza kujifunza upishi na kisha ikawa kwamba imebadilika kuwa kazi ilioipenda sana,” akaeleza Bi Nyambura.

Miaka ilipoasonga, Nyambura alipata mhisani aliyemlipia karo katika chuo cha mafunzo ya hoteli na upishi na baadaye akapata kazi katika hoteli moja mjini Nyeri.

“Nilikuwa nikifanya kazi mjini Nyeri na kurudi nyumbani wikendi katika kijiji cha Thunguma ili niwaone ndugu zangu. Haikuwa rahisi lakini nilijivunia kazi yangu,” akaongeza.

Wakati mmoja Bi Nyambura alisema alifiwa na mpwa wake na akiwa bado yuko kazini, watu wa familia walimtembelea na kumuuliza ikiwa angeenda nao kuuona mwili wa wendazake ambaye mwili wake ulikuwa katika chumba kimoja cha maiti katika hospitali ya Nyeri.

Wakati huo ndio ulikuwa mara yake ya kwanza kuzua chumba cha kuhifadhi maiti.

“Yale niliona kule yanisababisha nibadili nia maishani na nikaanza kuazimia kufanya kazi katika vyumba vya maiti. Mwili wa Mpwa wangu ulikuwa unaonekana vibaya sana, uliwachwa sakafuni na harufu ilikuwa ya kutisha,” akakumbuka Bi Nyambura.

Kulingana naye, alitamani sana kubadilisha kazi ili aishughulikie maiti na kuiweka katika hali nzuri.

“Mtu aliyeaga hawezi kujitetea na hata asipopata huduma ifaayo, ataozea mule ndani na kisha kuzikwa bila kupata haki,” akasema.

Hali hiyo ya kutamausha ilimkosesha raha Bi Nyambura kwa muda kabla ya kuamua kuigura kazi ya upishi na kujiunga na chuo cha mafunzo cha Chiromo ambacho ni mojawapo ya vyuo vya chuo kikuu cha Nairobi ambapo alisomea sayanzi ya chumba cha maiti. Picha/ Phyllis Musasia

“Watu wa familia hawakuamini uamuzi niliochukua na wengi wao walipinga sana uamuzi huo. Aliyenishika mkono ni ambaye sasa ni mume wangu na kila mara alinishauri nijikaze ili nitimize ndoto yangu,” akasema.

Nyambura hakuwa na fedha za kutosha kukamilisha masomo yake na alikumbuka sana jinsi mumewe alijizatiti na kuhakikisha kuwa amefuzu mnamo mwaka wa 2013.

Mara moja, Nyambura alipata ajira katika chumba cha maiti cha Chiromo ambapo alifanya kazi kwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja.

“Baadaye nilihamishwa hadi hospitali ya Nakuru Level Five ambapo kufikia wakati huu, nimehudumu kwa miaka 5,” akaeleza kwa tabasamu.

Akiwa mhudumu wa pekee wa kike katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo, wafanyikazi wenzake wanaenzi sana ujasiri alionao Nyambura. Kila mmoja alimsifia na kusema jinsi anavyofurahia kufanya kazi naye.

“Kila unapangwa kufanya kazi na Bi Nyambura, basi unakuwa na uhakikika kwamba kazi itafanyika vyema siku hiyo,” akasema Bw Erick Odhiambo, mfanyikazi mwenza wa Nyambura.

Mfanyikazi mwingine, John Maina alieleza kuwa bidii alionayo Nyambura ni kielelezo kwa watu wengi na mara nyingi wafanyikazi wa sehemu hiyo wamepokea zawadi nyingi kutoka kwa familia ambazo hurejea hospitalini kutoa shukrani zao kwa huduma nzuri ambazo hupokea.

“Yeyote ambaye hajapata fursa ya kutangamana na Nyambura, atakueleza kwamba ana roho safi kutokana na jinsi ambavyo yeye hujibeba,” akasema Bw Maina.

Kulingana naye, ujasiri alionao Nyambura, baadhi ya wafanyikazi wengine wa kiume hawana.

Nyambura hata hivyo alisema kufanya kazi katika chumba cha kuhifadhi maiti, haina tofauti na kufanya kazi nyingine ile. Kulingana naye, “kazi ni kazi bora mtu afurahie kazi anayoifanya na ifanye kwa dhati na bidii.”

“Jinsi nilivyokuwa mpishi ni vivyo hivyo ambavyo nahisi nikiwa mfanyikazi hapa. Tofauti ni mazingira ya kazi,” akaongeza.

Changamoto anazopitia ni pamoja na ajali ndogo ambazo hutokea wakati wa kupasua mwili.

“Unapata kwamba wakati fulani umejitaka na kisu ambacho unatumia kuupasua mwili na labda mtu huyo alikuwa na ugonjwa wa kuambukiza. Lazima upitie vipimo vya mara kwa mara na kuhakikisha kuwa unakunywa dawa,” akaeleza.

Baadhi ya kemikali ambazo pia hutumika kuhifadhi miili huwa hatari zinaposhika ngozi ya mhudumu. Pia wakati mhudumu anapovuta hewa ya kemikali hiyo inaweza kusababisha matatizo ya kupumua.

Nyambura alisema kila wakati mhudumu anapaswa kuwa makini na jinsi anavyovalia ili kuepuka ajali kama hizo.

“Mara tatu nimejipata nikitumia dawa za ARVS ili kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi baada ya kupata ajali wakati wa upasuaji wa miili,” akaongeza.

Kando na kazi yake ya kawaida, Nyambura pia huwazungumzia wale ambao wamesongwa na mawazo ya vifo vya wapendwa wao.

Mama huyo wa mtoto mmoja, anawasihi kina dada kujiunga na kazi sawia na yake na kwamba wasiwe na uoga.

Daktari msimamizi wa hospitali ya Nakuru Bw Joseph Mburu alisema chumba hicho cha maiti kina uwezo wa kuhifadhi maiti 84 kwa wakati mmoja.

You can share this post!

CORONA: ‘Ugonjwa huu umebana maisha yetu’

CORONA: Mahakama ya Milimani yasalia mahame

adminleo