Atakayerusha fataki kwa zaidi ya dakika 5 atakuwa taabani, wakazi Mombasa waonywa
EUNICE MURATHE Na WINNIE ATIENO
MBWEMBWE za kusheherekea Mwaka Mpya zitatatizika baada ya idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa kupiga marufuku fataki za usiku kucha.
Watakaokaidi agizo hilo wameonywa kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria serikali ya kaunti hiyo.
Wakazi wa Mombasa, watalii na wamiliki wa hoteli za fuoni wamekuwa wakikaribisha mwaka mpya kwa kuwasha fataki angani usiku kutwa.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki alisema watakaosherekea mwaka mpya wataruhusiwa kuwasha fataki kwa muda wa dakika tano pekee.
Kamishna huyo pia alionya kuwa mamaneja wa hoteli watachukuliwa hatua kali za kisheria endapo watakaidi agizo lake.
Fataki hutumika kwa sherehe kuahiria bahati nzuri au furaha.
“Kuna baadhi ya sehemu tumeziruhusu kuwasha fataki, lakini tumewapa muda wa dakika tano pekee, atakayepuuza agizo hilo basi atakuwa amevunja sheria,” akasema Bw Achoki.
Bila ya kutoa sababu za ‘kupiga marufuku’ fataki Bw Achoki aliwahakikishia wakazi kuwa usalama utadumishwa wakati wa sherehe hizo.
Alisema polisi wametumwa sehemu tofauto tofauti kushika doria na kuhakikisha usalama unadumishwa.
“Wale ambao wanadhania wataharibu amani na utulivu wa Mombasa watajipata pabaya manake kuna polisi wanafanya msako kila mahali” alisema.
Wawekezaji wa sekta ua utalii waliunga mkono ‘marufuku’ hayo wakisema haitozuia watalii kusheherekea mwaka mpya.
“Haitoathiri sherehe za mwaka mpya, watalii waliokuja Mombasa wamekuja kufurahia vivutio vyautalii,” alisema Bw Sam Ikwaye afisa mkuu wa muungano wa wahudumu wa hoteli.
Haya yanajiri huku serikali ya kaunti ya Mombasa ikipania kufanya sherehe za mwaka mpya kwa kuwasha fataki ambapo waimbaji maarufu wanatarajiw akutumbuiza wakazi akiwemo Ali Kiba.
Mamia ya wakazi wanatarajiwa kumiminika bustani ya Mama Ngina kwa shehere hizo za mwaka mpya.
Rais Uhuru Kenyatta angali Mombasa.